NA VICTORIA GODFREY

UONGOZI wa Chama cha Mpira wa Wavu Mkoani Mbeya (MBEREVA) umesema una mpango wa kuwekeza ngazi ya mitaa mkoani humo.

Akizungumza na Zanzibarleo Katibu Mkuu wa MBEREVA Pascal Obeid, alisema lengo ni kuhakikisha mchezo huo unachezwa na watu wa rika zote.

Alisema timu nyingi zinatoka katika taasisi za Majeshi,hivyo mpango ni kubadilisha kuhakikisha unachezwa na timu za kiraia kwa wingi.

” Tunataka kuanzia ngazi ya mitaa ili kuhakikisha kunakuwa na timu za kutosha na mchezo huu uchezwe na watu wa kawaida na sio kama ulivyozoeleka kuona timu za taasisi za Majeshi”, alisema Obeid.

Alisema mpango mwingine ni kuhakikisha mchezo huo unafika katika skuli mbalimbali mkoani humo, kwa kuendesha mafunzo kwa walimu wa michezo ambao watatumika kuibua na kuendeleza vipaji katika vituo vya kazi zao.

Katibu huyo alisema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha, hivyo bado wanapambana kuhakikisha wanazungumza na wadau wa michezo mkoani humo waweze kuwaunga mkono kukabiliana na changamoto hiyo.