ZASPOTI
KLABU ya Paris St-Germain inafanya mazungumzo na wawakilishi wa Lionel Messi juu ya mshambuliaji huyo wa Argentina kujiunga na miamba hiyo ya ‘Ligue 1’ kufuatia kuondoka Barcelona.
Kambi ya Messi iliwasiliana na PSG mara tu ilipobainika kuwa Barcelona haiwezi kuheshimu mkataba waliokubaliana.

Mazungumzo zaidi yalifanyika juzi yakilenga kuongeza mpango huo kwa kuwaweka pamoja.
Wiki iliyopita, miamba hiyo ya Kitalunya ilisema, Messi, wakala huru, hatabakia klabuni hapo.
Ilishutumu ‘vizuizi vya kifedha na kimuundo’ kwa mchezaji huyo kuondoka baada ya miaka 21.

Baadaye, rais wa Barca, Joan Laporta, alisema, kumbakisha Messi kungeweza kuiweka klabu kwenye hatari kwa miaka 50.
Messi (34), amekuwa wakala huru tangu Julai 1 wakati mkataba wake ulipomalizika. Alikuwa amekubali kandarasi mpya ya miaka mitano juu ya mshahara uliopunguzwa, lakini, klabu ilibidi ipunguze bili yao ya mshahara ili kumudu, na haikuweza kufanya hivyo.

Nahodha huyo wa Argentina ndiye kinara wa rekodi ya ufungaji Barcelona akiwa na magoli 672 na ameshinda mataji 10 ya La Liga, manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na saba ya Copa del Reys, na pia kuweka rekodi mara sita ya kutwaa tuzo ya ‘Ballon d’Or’.

Bosi wa Barca, Ronald Koeman, alisema, anamtakia mema Messi.
Inahisiwa Messi yuko sawa na wazo la kujiunga na PSG, ikizingatiwa anawajua tayari wachezaji wao kadhaa.
Neymar alichezea Barcelona kutoka 2013-2017 kabla ya rekodi yake ya ulimwengu ya pauni milioni 200 kuhamia PSG, na Messi anabaki karibu na Mbrazil huyo.(Marca).