PARIS, Ufaransa
LICHA ya kuanza kufanya mazoezi na timu, Paris St-Germain haijafanya uamuzi wa kumtumia nyota wa Argentina, Lionel Messi kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’. PSG jana ilitarajiwa kuchezwa na Brest.

Messi, mshindi wa tuzo ya ‘Ballon d’Or mara sita, akiwa na umri wa miaka 34, amekubali kujiunga na PSG kama mchezaji huru kufuatia kudorora kiuchumi kwa Barcelona kulikochagizwa na ‘corona’.

Nyota huyo hajacheza mechi yoyote tangu alipoisaidia timu yake ya taifa ya Argentina kushinda ubingwa wa Copa America mbele ya Brazil.
“Hatujafanya uamuzi bado kama Messi atacheza au laa”, alisema, kocha Mauricio Pochettino.

“Kila kitu kiko sawa kwenye malengo chanya, kuna hali nzuri kwenye kikosi”.
Katika hatua nyengine, kocha huyo wa matajiri hao wa jiji la Paris, Pochettino, amesema, mshambuliaji wake, Kylian Mbappe, hataondoka msimu huu, licha ya kuhusishwa kujiunga na miamba ya soka la Hispania, Real Madrid.
Wakati huo huo, gwiji wa mpira wa kikapu, Michael Jordan hadi sasa amepata karibu dola milioni sita kutoka kwenye jezi za PSG zilizouzwa kwa jina la Lionel Messi, kwa mujibu wa MARCA.

Kulingana na chanzo hicho, Jordan anapata asilimia 5% kwa jezi yoyote inayouzwa na PSG kwani miamba hiyo ya PSG inadhaminiwa na chapa ya Nike ya Air Jordan.
Kwa hali ilivyo, kuwasili kwa Messi jijini Paris kumeipatia PSG karibu euro milioni 120 kupitia mauzo ya jezi kitu ambacho kinamaanisha Jordan ametia mfukoni karibu kiasi hicho cha fedha.

Kulingana na Forbes, nyota huyo wa zamani wa Chicago Bulls alipoteza utajiri wake mwingi kutokana na janga la ‘corona’. Jordan inasemekana amepoteza karibu asilimia 24% ya thamani yake ambayo imepungua kutoka dola bilioni 2.1 hadi 1.6.

Messi ni mchezaji wa pili anayeuza zaidi baada ya Cristiano Ronaldo. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34 amejiunga na PSG kwa mkataba wa miaka miwili na chaguo la kuongeza mwaka mwengine.

PSG inaweza kutarajia kuuza jezi nyingi zaidi ya chapa ya Air Jordan katika siku zijazo zinazoonekana, ambayo nayo pia itamnufaisha Jordan. (Goal).