NA VICTORIA GODFREY

MFALME wa mashindano ya soka ya ndondo cup anatarajia kupatikana leo katika fainali itakayochezwa  kwenye Uwanja wa Bandari Tandika Dar es Salaam.

Fainali hiyo itazikutanisha Tabata All Star watavaana dhidi ya Vifundo FC katika mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba hilo.

Akizungumza na Zanzibar leo Msimamizi wa  Mashindano hayo,  Ally Kulita, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kwamba hali ya uwanja, ulinzi na usalama vipo vizuri .

“Tunashukuru Mungu tumekamilisha maandalizi yote kwa weledi mkubwa na kesho (leo) tunatarajia kupata mfalme wa mashindano haya,” alisema Kulita.

Naye Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo kutoka chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Daud Kanuti,alisema matarajio ni kuona ushindani mkubwa kutokana na kila mmoja atakuwa amejiandaa vizuri.

Aliwaomba mashabiki na wapenzi kujitokeza kwa wingi na kuzingatia taratibu za kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona pamoja na kuwa na nidhamu uwanjani.

“Tunawatakia Kila heri katika mchezo wa (kesho) leo,matumaini yetu kila mmoja amejiandaa na matokeo uwanjani ndio atatupa Bingwa wa mwaka huu,” alisema Kanuti.