YAMOUSSOUKRO,IVORY COST

WIZARA ya afya ya Ivory Coast imesema msichana raia wa Guinea aliyekutwa na virusi vya Ebola baada ya kuwasili nchini humo wiki mbili zilizopita amepona ugonjwa huo.

Mkuu wa taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Ivory Coast Serge Eholie,alisema kuwa walimfanyia vipimo mgonjwa huyo na baada ya saa 48, vipimo vilionyesha kuwa amepona ugonjwa huo wa kuharisha na kutapika damu.

Msichana huyo raia wa Guinea ndio alikuwa mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Ebola kugunduliwa nchini Ivory Coast tangu mnamo mwaka 1994.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 18 alikuwa amesafiri kwa basi hadi Abidjan kutoka Labe kaskazini mwa Guinea, safari ya takriban kilomita 1,500 inayopitia eneo lenye msitu mkubwa ambapo mripuko wa maambukizi ya Ebola uliripotiwa mapema mwaka huu, na pia kati ya mwaka 2013 hadi 2016.

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kisa hicho cha ebola ni jambo la kutia wasiwasi kwa kuwa kimetokea katika eneo lililokuwa na zaidi ya watu milioni nne.