NA ABOUD MAHMOUD
PAZIA la michuano ya kuwania kombe la mashirika linatarajiwa kufunguliwa leo katika dimba la Mao Zedong mjini Unguja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa muandaaji wa mashindano hayo Abdullah Thabit ‘Dulla Sunday’ alisema ufunguzi huo unatarajiwa kuanza majira ya saa 1:00 usiku.
Mratibu huyo alisema katika mechi ya ufunguzi timu ya Global hospital watavaana na Taasisi ya Viwango.
“Mashindano yetu ya mashirikia yataanza leo na mechi ya ufunguzi itakua kati ya Global hospital na Taasisi ya Viwango, “alisema.
Mratibu huyo alisema mashindano hayo yamegawika makundi A mpaka D.Sunday alisema kundi A litakua na timu ya Global hospital,Taasisi ya Viwango na ZECO.
Kundi B timu ya Vigor,PBZ na ZRB huku kundi C likiwa na timu Umoja wa Ndege ndogo,Al Rahma Hospital na Azam.
Kwa upande wa kundi D timu zitakazoshiriki ni TRA, Raskazone na Amana Bank.Aidha mwandaaji huyo alifahamisha kwamba mechi hizo zote zitachezwa Mao Zedong majira ya usiku.
Sambamba na hayo Sunday alieleza kuwa katika mashindano hayo bingwa atajinyakulia kitita cha shilingi 1,000,000, mshindi wa pili ataondoka na 500,000.