NA SABRA MAKAME,SCCM

MKURUGENZI Mipango, Sera na Utafiti Ofisi ya Rais Fedha na Mpango, Saumu Khatib Haji, amesema zoezi la uhakiki  kampuni ya Master Life Microfinance  Limited imekua changamoto ukilinganisha na Kaskazini kutokana na mikataba mingi kuwa na mashaka kwa wamiliki.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo Ziwani Polisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi uwanja wa Bomani wakati zoezi la uhakiki likiendelea.

Alisema kumekua na changamoto kubwa kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa Mjini Magharibi kutokana na wananchi wengi kutokuonekana katika mfumo wa usajili wa Master Life.

“Mikataba mingi ya mjini haina picha ya muhusika, kitambulisho na vile vile katika ‘finance manager’ kuna saini tofauti tofauti ,kwa kweli zoezi kwa mjini lina changamoto nyingi”alisema mkurugenzi

Mkurugenzi alisema kwa kila mikataba ambayo ina changamoto wanachukua jitihada ya kurikodi kuhakikisha wanawasaidia wananci kwa namna moja ama nyengine.

Saumu alisema, kumekuwa na mikataba ambayo haihusiki katika uhakiki huo, lakini kuna baadhi ya wananchi wameiingiza katika mzunguko.

Vile vile aliwashauri wananchi kuwa waangalifu  katika kipindi chote cha uhakiki, ili kuenda sambamba na ratiba ambazo zimeekwa.

Zubeda Hassan Muhammed, mkaazi wa Mkamasini alisema alishiriki katika zoezi la uhakiki na kugundulika kuna saini  feki ya bosi.

“Kwanini Master Life wanamiliki vibali vya kuwahalalisha wafanye kazi , wanatumia jengo la serikali kufanyia biashara ambayo ni feki, lazima kutakua na baadhi ya wafanyakazi wamekula rushwa lazima serikali ichukue hatua inayostahili”alisema Zubeda