NA KHAMISUU ABDALLAH

TAASISI ya Milele Zanzibar Foundation imekabidhi boti na mashine ya uokozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 10 kwa wavuvi wa kijiji cha Mangapwani.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi boti hiyo huko Mangapwani Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Kassim Mbaruk Juma, alisema lengo la kupelekea boti hiyo ni kusaidia shughuli za uokozi na masuala mbalimbali yanayojitokeza katika bahari.

Alisema boti hiyo ina urefu wa futi 24 na uwezo wa kuchukua watu 40 kwa wakati mmoja ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa kijiji hicho kuweza kufanya shughuli za uokozi pale yanapotokezea maafa ya watu kuzama baharini.

Aidha alisema kutolewa kwa chombo hicho ni muendelezo wa tasisi yao katika kuendelea kutekeleza masuala ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Aliishukuru kamati ya maendeleo ya jimbo la Bubwini kwa kukubali kupokea msaada hiyo na kuamini kwamba chombo hicho kitatunzwa na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na sio kwa shughuli nyengine ikiwemo za ubebaji wa mizigo na abiria kutoka sehemu moja kwenda nyengine.

Alieleza kuwa taasisi ya milele itaendelea kusaidia wananchi katika shughuli za kimaendeleo kila panapohitajika kwa lengo la kuisaidia serikali kuharakisha upatikanaji wa shughuli za maendeleo kwa Zanzibar.

Mbunge wa Jimbo la Bubwini Mbaruk Juma Khatib, aliishukuru tasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa kuwasaidia boti hiyo ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa kijiji hicho.

Hivyo, aliwataka kuitunza boti hiyo na kuwa na umoja na mshikamano katika kuendeleza shughuli za uokozi na kuahidi kutoa ushirikiano na kamati ya uvuvi ili iweze kufanya kazi zake vizuri ili kuwapa moyo wahisani wao kuweza kuwasaidia mambo mengine.

Nao wananchi wameshukuru kupatiwa Kwa boti hiyo kwani imewarahisishia kuondosha matatizo yanayojitokeza katika shughuli za uokozi.