NA HAFSA GOLO

MSTAHIKI Meya Baraza la Manispaa Mjini, Ali Haji Haji, amesema wamo katika hatua ya utekelezaji ya  mpango mpya  mkakati wa kuimarisha usafi wa mazingira katika mji wa Zanzibar.

Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Malindi mjini Unguja, alisema mpango huo unawashirikisha Madiwani na watendaji wote wa baraza hilo ambao hufanyika katika maeneo sugu ya  uchafu mji huo kwa kila siku za Jumamosi.

“Baadhi ya maeneo yaliokithiri uchafuzi wa mazingira katika mji wa Unguja ni  pamoja na Magomeni, Sogea, Jangombe, Kwahani na Kwaalinatu”,alisema.

Aidha, alisema mpango huo upo sambamba na utekelezaji wa uanzishaji wa vikundi maalumu vya usafi katika maeneo hayo sugu lengo ni kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya mazingira.

Hata hivyo, alisema kupitia mpango huo kwa sasa umesaidia kuleta mabadiliko na hatimae mji wa Zanzibar kuonekana katika sura inayoridhisha.

Meya huyo, alisema pamoja na mafanikio yaliofikiwa Baraza hilo halitosita kumchukulia hatua za kisheria mwananchi yoyote atakaebainika kuhusika na ukiukwaji wa sheria za kuhifadhi na kulinda mazingira ya mji.

Katika hatua nyengine aliwasihi wananchi kubadilisha tabia ya kupenda usafia na kuchukia uchafuzi wa mazingira kwani kufanya hivyo itasaidia kufikia malengo ya serikali katika suala zima la usafi wa mazingira.

Mapema Meya alisema kwamba baraza hilo hivi sasa limekuwa likifatilia kwa karibu mbinu mbali mbali zinazotumiwa kwenye miji mengine ambayo imepiga hatua za mafanikio ya uimarishaji wa usafi ikiwemo Arusha.

Wakati huo huo, Meya huyo, alisema Manispaa ya Mjini limepata mashine 10 za kisasa kwa ajili ya udhibiti wa  ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuzuia uvujaji wa mapato ndani ya baraza hilo.

“Serikali ya awamu ya nane imetuagiza kusimamia maeneo muhimu matatu moja ni kuhakikisha mji unakuwa safi, tutenge maeneo rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na tuhakikishe tunakusanya mapato kwa utaratibu mzuri na kuzuia yasivuje”, alisema,