NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

KIUNGO wa timu ya Simba SC, Jonas Mkude amerejea kambini na baadhi ya wachezaji wanzake wa kikosi hicho ambao walikuwa mapumzikoni.

Kabla ya kumalizika kwa ligi kuu Tanzania Bara kamati ya nidhamu ya klabu iliwaagiza viongozi kumfanyia vipimo vya kiafya katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba baada kupata taarifa za kitabibu ndio kamati itatoa uamuzi wa mwisho juu ya mchezaji wao huyo.

Hiyo ni baada ya kamati kupokea mashtaka mawili ya utovu wa nidhamu ya mchezaji Mkude, ambapo walikaa na kusikiliza pande zote mbili kwa mchezaji na timu hiyo.

Hivyo kwa kuzingatia mazingira yanayohusiana na mashauri ya mchezaji Jonas Mkude, kamati iliomba viongozi wa Simba kumfanyia vipimo mchezaji wao.

Jana klabu ya Simba kupitia ukurasa wao wa kijamii waliweka picha ya Mkude na kuandika amerudi kambini pamoja na picha za wachezaji mbali mbali.