NA ABOUD MAHMOUD

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema Serikali inaedelea na mikakati ya kuweka miundombinu ya kuzuia uharibufu wa fukwe za bahari .

Hayo aliyasema wakati alipokutana na watendaji wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiongozwa na Waziri wake Balozi Lebarata Mulamula huko ofisini kwake Migombani.

Dk. Mkuya, alisema mikakati hiyo ni pamoja na kuweka kuta ambazo zitasaidia kuzuia mmong’onyoko wa ardhi unaosababishwa na kupanda kwa kina cha maji ya bahari.

“SMZ kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambao ndio wanaoshughulika na maswala ya mazingira tunaendelea na mikakati ya kuweka miundobinu katika fukwe za bahari,”alisema.

Alisema hatua hiyo inatokana mabadiliko ya tabia nchi inayotokana na uharibifu unaofanywa na wananchi katika fukwe za bahari nchi kavu na tayari wameshaanza kujenga ukuta katika bandari ya Msuka Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba.

Kuhusu udhibiti wa dawa za kulevya, Dk. Mkuya, alisema kwamba wameandaa mpango wa kueka vifaa maalum vya kukagulia wageni na mizigo inayoingia nchini ikiwa lengo ni kudhibiti dawa hizo , kwani mizigo mingi inayoingia nchini haifanyiwi ukaguzi wa kitaalamu.

Nae, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Lebarata Mulamula, amesema Wizara yake itaendeleza ushirikiano uliopo kwa ajili ya maendeleo ya taifa na kuimarisha masuala ya mazingira na kuahidi kufanya ziara za mara kwa mara, ili kujifuza zaidi.

“Nikuahidi kuendeleza mashirikiano baina ya Wizara yangu na yako kwa lengo la kujifunza mambo mbali mbali na kufikia malengo yatakayosaidia taifa kwa ujumla,”alisema.