WASHINGTON, MAREKANI

WATAALAMU wa mabadiliko ya tabianchi wa Marekani wametabiri kuwa, moto mkubwa utaendelea kuteketeza maeneo ya magharibi mwa Marekani na kuongezeka kwa joto ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi duniani.

Wataalamu hao na maofisa wa zima moto walitabiri kuwa, maeneo ya magharibi mwa Marekani yataendelea kuathiriwa na moto mkubwa kwa kuzingatia hali ya joto kali inayotawala sasa.

Kwa sasa maofisa wa Idara ya Zima Moto na wa majimbo ya Marekani wanajiandaa kukabiliana na moto mkubwa unaotarajiwa kuyaathiri maeneo ya kaskazini na kaskazini magharibi mwa jimbo la California.

Televisheni ya CNN imeripoti kuwa, hadi  Jumanne wafanyakazi wa huduma ya zima moto zaidi ya elfu 26 walikuwa wamefika katika majimbo 15 ya Marekani kwa ajili ya kuzima moto mkubwa ambao hadi sasa umeteketeza zaidi ya hekta elfu moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, moto mkubwa wa sasa ulioiathiri Marekani ambao umepewa jina “Dixie” unatajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya California.