ROME, Italia
KOCHA wa AS Roma, Jose Mourinho, ameanza na ushindi katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Europa dhidi ya Trabzonspor ya Uturuki.

Nahodha, Lorenzo Pellegrini, aliwapa uongozi Roma wakati alipokwamisha mpira nyavuni akimalizia krosi maridhawa ya kiungo mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Arsenal, Henrikh Mkhitaryan.

Akitokea benchi, Andreas Cornelius alifunga goli la kusawazisha kwa Trabzonspor, lakini, goli la mshambuliaji, Eldor Shomurodov liliwapa utawala Roma na kumaliza vyema raundi ya kwanza ya mtoano huo ikishinda 2-1.

Roma inaweza kufuzu kucheza hatua ya makundi endapo itashinda au kufungwa chini ya goli moja, lakini, watakosa nafasi hiyo kama watafungwa kwenye mchezo utakaopigwa dimba la Stadio Olimpico Roma wiki ijayo.

Mourinho ameshinda mataji mbali mbali akiwa Chelsea, Manchester United, Inter Milan kasoro Tottenham kabla ya kuchukua mikoba ya kuinoa Roma iliyokuwa chini ya Paulo Fonseca.Kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya ‘Serie A’, Roma itamenyana na Fiorentina kesho.(Goal).