NA MADINA ISSA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imetiliana saini na taasisi ya kimataifa inayoshughulikia masuala ya elimu kwa wote kutoka Qatar mtakaba wa makubaliano mradi wa kuwarejesha madarasani watoto waliotoroka skuli.

Mkataba huo wenye lengo la kuwarejesha skuli watoto wapatao 36,000 walioacha masomo, umesainiwa na Katibu Mkuu wizara ya Elimu Zanzibar, Ali Khamis Juma na Mwakilishi kutoka taasisi ya Elimu kwa wote ya Qatar, Dk. Marry Pigozzi hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa hoteli ya Park Hayat.

Akizungumza mara baada ya saini hiyo, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said, alisema, watahakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu kuanzia ngazi ya maandalizi hadi kidato cha nne.

Hivyo, alisema, mradi huo utasaidia kufikiwa kwa malengo hayo na kusema kuwa mkataba huo ni muhimu na serikali itatoa msukumo wa ziada kuona unafanikiwa kwani mbali ya kuwapatia elimu watoto pia utaipunguzia serikali mzigo.

Aidha alifahamisha kuwa watakuja na mikakati tofauti ili kuona mtoto anarudi skuli na kuendelea na masomo yake ambayo yatakuwa msingi katika maisha yake ya baadae.

Hivyo, waziri Simai alisema, tayari wameshafanya majaribio katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo watoto waliotoroka masomo yao wameanza kurejea madarasani.

Naye, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Education Above all la Qatar, Dk. Marry Pigozzi, alifahamisha kuwa mpango wa elimu kwa wote unaendeshwa na taasisi yao una lengo la kuwafikia watoto waliotoroka na kuacha masomo yao wakiwemo wenye mazingira magumu.

Mapema Mkurugenzi Sera, Mipango na Utafiti kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Masudi, alisema tayari mradi huo umezinduliwa na unaendelea vyema katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo takribani watoto 4,000 wanaendelea na masomo kupitia mradi huo.

Hivyo, alisema wataendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali wakiwemo masheha, wakuu wa wilaya na Mkoa, kwa kuhakikisha watoto hao wanapatikana na wanarudi skuli.

Katika utekelezaji wa mkataba huo watoto wenye umri wa miaka 7 hadi 17 waliacha skuli kwa matatizo mbalimbali watarejeshwa skuli kwa kuwajengea mazingira rafiki, miundombinu bora ya usomeshaji Unguja na Pemba.

Jumla ya dola milioni 3 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mradi wa kuwarejesha skuli ambao watoto 36,000 wanatarajiwa kurejeshwa skuli chini ya ufadhili wa shirika la UNICEF pamoja na taasisi ya elimu kwa wote ya Qatar.