NA HASHIM KASSIM

SHIRIKISHO la mchezo wa nage Zanzibar (SHINAZA) pamoja na wadau wa mchezo huo, wametakiwa kufuata katiba na kanuni zao katika kufanya maamuzi.

Wito huo ulitolewa na Mrajisi wa vyama vya Michezo Zanzibar Abubakar Mohammed Lunda, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwanakwerekwe.

Alisema baada ya kufanya uchaguzi na kupata viongozi watakao ongoza mchezo huo, aliwataka viongozi kuisoma na kuielewa katiba yao ili kujiepusha na migogoro.

“Chama kikisajiliwa muongozo wetu ni katiba kwa hiyo kwa viongozi waliochaguliwa na wanaongozwa, lazima wawe na uelewa na katiba yao hata kiongozi akikosea tunaangalia vifungu vinasemaje” alisema Lunda.

Shirikisho hilo lilifanya mkutano mkuu mwishoni wa wiki iliyopita ulioambatana na uchaguzi wa viongozi wa ngazi za taifa huku Aisha Omar Yussuf akichaguliwa kuwa rais wa mchezo huo.

Mbali na hayo wajumbe watatu walichaguliwa katika mkutano huo ambao ni Lutfia Ameir, Tatu Abeid na Abdallah Khatibu, Nage inakabiliwa na mashindano mbalimbali ikiwemo Mapinduzi cup na kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi.