NA ZUHURA JUMA

MSHITAKIWA Nassor Issa Nassor (30) mkaazi wa Kizimbani Wete, amedai kuwa hana hakika iwapo alimuingilia mtoto wa kike wa miaka tisa kinyume na maumbile, kwa sababu anaugua ugonjwa wa wasi wasi mara kwa mara.

 Mshitakiwa alitoa madai hayo  katika mahakama ya mkoa  Wete, wakati akijitetea kutokana mashtaka yanayomkabili.

Alidai anachokikumbuka walikwenda askari polisi nyumbani kwao na kumchukua bila kujua kosa alilofanya.

Alidai hakupinga kuwafuata lakini walipoanza kumpiga aliwauliza kosa lake na kujibiwa kuwa akifika kituo cha polisi ataambiwa kosa lake.

Alidai baada ya kufika aliambiwa kuwa, alimdhalilisha kinyume na maumbile mtoto wa miaka tisa, jambo ambalo yeye alidai hakulifanya.

Alidai  anapofanya jambo huwa hajijui kwani ni mgonjwa wa wasiwasi tangu alipokuwa mdogo na amepelekwa hospitali na wazazi wake lakini bado hajapona.

“Naugua maradhi ya wasiwasi tangu nilipokuwa mdogo, hata ninalolifanya silijui mie, baba kanipeleka hospitali mara nyiungi lakini sijapona,” alisema.

Baba mzazi wa mshitakiwa, Issa Nassor, alipoulizwa na hakimu wa mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamhun kuhusu ugonjwa wa mtoto wake alidai mwanae ni mgonjwa wa akili tangu alipokuwa darasa la saba.

“Aliacha kwenda skuli kwa ugonjwa huo na tumekwenda hospitali ya Wete, Chake Chake, Mkoani, Kidongochekundu na Dar es Salaam lakini hatujafanikiwa,” alidai.

Alidai kuwa, wakati mwengine anakuwa vizuri kiakili lakini wakati nyengine anakuwa mgonjwa wa kupita majaani na kuokota makopo.

Hata hivyo, baba huyo hakuwa na kielelezo chochote cha hospitali cha kuithibitishia mahakama kwamba mwanae mgonjwa.

“Mheshimiwa hakimu leo sina vielelezo hapa nimevisahau, lakini vikihitajika nitakuja navyo,” alidai.

Baada ya utetezi huo, aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 31 kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa alitenda makosa mawili; kosa la kwanza alilitenda Julai 26 mwaka jana saa 1:30 za usiku katika shehia ya Bopwe Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Ilidaiwa kuwa, bila ya halali na bila ya ridhaa ya walezi wake alimtorosha mtoto huyo kutoka nyumbani kwao na kwenda nae migombani jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kosa la pili alimuingilia kinyume na maumbile mtoto huyo mwenye miaka tisa, jambo ambalo ni kosa kisheria.