NA ABOUD MAHMOUD

MSANII wa muziki wa taarab nchini Tanzania, Sabah Khamis Said (Sabah Muchacho), anatarajiwa kupanda jukwaani katika tamasha la ‘Zuchu Home Coming’, linalotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu katika uwanja wa Amaan.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia nya simu akiwa jijini Dar es Salaam msanii huyo mkongwe, alisema lengo la kushiriki tamasha hilo ni kumuunga mkono msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya ambae pia ndie muandaaji wa tamasha hilo.

‘’Ni kweli kama ulivyosikia natarajia kwa uwezo wa Mungu na mimi kushiriki katika tamasha linaloandaliwa na mwanangu Zuchu, lengo ni kumuunga mkono na kuonesha umuhimu wa sanaa katika jamii yetu,” alisema.

Sabah alisema anafahamu kwamba katika tamasha hilo wengi watakaojitokeza ni wapenzi wa muziki wa kizazi kipya, lakini na wa muziki wa taarab pia watakuwepo.

Alisema kwamba ushiriki wake katika tamasha hilo utaleta burudani tosha kutokana na kuwepo kwa burudani ya muziki wa kizazi kipya na taarab.

“Vijana wengi wanapenda muziki wa kizazi kipya na wengi wanampenda Zuchu lakini na wanaopenda taarab za kisasa wapo wengi na ndio nikaamua nije ili kulinogesha na kulifanya liwe tamasha la ladha tofauti,” alisema.

“Siku nyingi sana Zanzibar sijaimba kwenye taarab za kawaida naimba kwenye harusi tu, nawaomba mashabiki wangu kuja kwa wingi Agosti 21 ili kupata burudani mwanana itakayokonga nyoyo zao,” alifafanua.

Sabah Muchacho ni miongoni mwa wasanii mahiri wa muziki wa taarab anaetamba na nyimbo mbali mbali, ikiwemo ‘Niacheni nijivune, Mlango wa Mungu, fimbo ya Mungu, Chakubimbi, Semeni na nyengine nyingi.