NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha CUF Zanzibar, Abbas Muhunzi Shaame, ametangaza kurejea kwenye nafasi hiyo, akidai kufukuzwa ilikuwa kinyume na katiba cha chama hicho.

Muhunzi alifukuzwa nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa kukiuka maadili ya uongozi mwezi Juni mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisi za CUF, Kilimahewa, alisema, amemaliza mapumziko ya ugonjwa na sasa anarejea kwenye nafasi hiyo na kuendelea na shughuli za kukitumikia chama hicho.

Alisema, kwa mamlaka aliyopewa na katiba kama kiongozi mkuu wa shughuli za chama upande wa Zanzibar, ameteua Hamida Huweishi, kufanya shughuli za ukatibu mkuu huku Ali Makame Issa akiwa Naibu Katibu Mkuu.

Alisema, kwa ajili ya kuunganisha nguvu ya kufufua chama, amempendekeza Khamis Mohammed Faki kuwa mratibu wa chama kati ya Unguja na Pemba.

Wengine walioteuliwa ni Dhifaa Mohammed Bakari (Mwenyekiti wa Wazee) na Mtumwa Ambar Abdalla (Mwenyekiti wa Wanawake).

Alisema, jukumu kubwa atakalolifanya kwa sasa baada ya kurejea madarakani ni kurejesha hamasa ya wananchama iliyopotea baada ya mgogoro mkubwa uliokikumba chama hicho na kusababisha vigogo kadhaa kuondoka na kuhamia ACT-Wazalendo.

Makamu huyo, alisema, kwa mujibu wa katiba ya CUF, kifungu 11(6) ni haki ya mwanachama kujitetea mbele ya chombo chochote cha Chama kinachotaka kumchukulia hatua za kinidhamu, lakini, yeye hakupewa fursa hiyo wakati akifukuzwa.

“Nasikitika mimi sikuitwa na mkutano mkuu kujieleza licha ya kwamba nilijigharamia  na kuwa karibu mkutono kungojea kuitwa”, alisema.

“Niliwapigia simu wajumbe wa mkutano mkuu na kuwaeleza nipo nje, lakini, nikitakiwa nitakuja”.Lakini, alisema, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, aliamua kinyume na matakwa ya katiba.