ZASPOTI
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ametoa zawadi ya magari na nyumba kwa wanamichezo wa nchi hiyo walioshinda medali katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika mjini Tokyo, Japan.

Uganda ilipeleka wanamichezo 25 kwenye michuano hiyo, na kufanikiwa kushinda medali nne, mbili za dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba.
Mwanariadha, Joshua Cheptegei aliyeshinda medali ya fedha katika mbio za mita 10,000 na kushinda dhahabu katika mbio za mita 5,000 alipewa Mitsubishi Pajero Sport.

Naye, Peruth Chemutai aliyeshinda medali ya dhahabu katika ‘steeplechase’ mita 3,000 alipewa Parejo Sport ya bluu na Jacob Kiplimo aliyeshika nafasi ya tatu na kushinda medali ya shaba kwenye mbio za mita 10, 000 amepewa Pajero Sportero L200 ya kijivu.

Baada ya kukabidhi zawadi za magari, Rais Museveni, akaahidi kuwajengea nyumba wazazi wa washindi wa medali za dhahabu.
Pia washindi hao watakuwa wakilipwa mshahara kwa mwezi.
Washindi wa medali za dhahabu watalipwa dola 1, 420 kwa mwezi, washindi wa medali za fedha watalipwa dola 851 na washindi wa medali za shaba watalipwa dola 283. (Daily Monitor).