NA ALI MAHFOUDH, (TUMAINI) 

MWAKILISHI wa Jimbo la Bububu ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Soraga, amesema uongozi wa jimbo upo tayari kuanza ujenzi wa miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo, ili kufikia malengo ya fedha za mfuko wa Jimbo walizopokea kutoka serikali kuu

Akizungumza na Waandishi wa Habari,  jana  mara baada ya kukamilisha ziara katika shehia sita za Jimbo hilo, ambapo amesema amepokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wananchi juu ya miradi wanayoipa kipau mbele  kutekelezwa kwa awamu ya kwanza katika kila shehia.

Alisema ziara hiyo wananchi wa shehia ya Dole wamependekeza ujenzi wa matundu ya vyoo katika skuli ya msingi Dole, kwani ni changamoto kubwa kwa wanafunzi katika shehia hiyo.

Upande wa shehia ya Bububu alisema wananchi wamependekeza ujenzi wa daraja, katika shehia ya Kijichi ambao wametaka ukarabati wa maktaba katika skuli ya msingi na sekondari Kijichi, ikiwa pamoja na changamoto kubwa kuvuja kwa paa la jengo hilo.

Ameongeza kua katika shehia ya Kizimbani wananchi wamependekeza ujenzi wa fremu za maduka, ili kuendeleza ujasiriamali, na  eneo la Mbuzini wamependekeza fedha hizo zitumike kuongeza nguvu katika ujenzi wa skuli ya maandalizi Mbuzini, ili uweze kukamilika kwa wakati, na  Chemchem wametaka kujengewa daraja dogo la Kigamboni kwa Bihamida.

Kuhusu miradi mikubwa iliyochini ya nguvu za serikali ukiwemo wa Ujenzi wa Daraja la Sakafuni na Umeme kutokana na trasfoma iliypo kuzidiwa,  Soraga alisema atayafikisha katika serikali kuu, ili yaweze kufanyiwa kazi.

Nae, Diwani wa Wadi ya Dole, Juma William Sungwa, ameshauri Mamlaka ya Maji kuliangalia tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji katika chemu chemu ya Bububu, ili wananchi waweze kuyatumia.

” Kuhusu changamoto ya maji ni kubwa Sana, lakini tuna pendekezo kwamba kunaweza kuwa na miundombinu rahisi ya kuyakusanya maji yanayotiririka kutoka kwenye chemechem yetu hii”