NA HAFSA GOLO

TATIZO la ukosefu wa vitega uchumi vya uhakika linachangia kutokipatia Chama cha Mapinduzi (CCM) mapato ndani ya jimbo la Paje.

Mwakilishi wa jimbo hilo, Dk. Soud Nahoda, alieleza hayo wakati alipokua akiwasilisha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025 katika kipindi cha miezi sita hafla iliyofanyika jimboni humo.

Alisema suala hilo linapelekea kujitokeza kwa changamoto za kiutendaji katika jumuiya mbali mbali za chama hicho zilizopo ndani ya jimbo la Paje.

“Kutokuwepo kwa vitega uchumi vya uhakika ndani ya jimbo letu tu nakosa kukipatia chama chetu mapato na kuendesha vizuri jumuiya zetu ndani ya jimbo letu” alisema.

Alisema tatizo hilo linachangia kutoweza kuyafanyia ukarabati matawi ya CCM yaliomo jimboni humo ili yaendane na hadhi ya Chama chenyewe.

Hivyo Mwakilishi huyo alisema ni vyema viongozi wa jimbo hilo kushirikiana kwa pamoja kutafuta mbinu mbadala za kushajihisha wanaCCM jimboni humo kubuni vitega uchumi endelevu vitakavyosaidia uimarishaji wa mapato.

Alisema kuwepo kwa vitega uchumi vya uhahika ndani ya chama itasaidia kuleta mageuzi ya kiutendaji ndani ya CCM jimboni humo.

Akizungumzia kuhusu mashirikiano, Dk. Soud, alisema ni vyema viongozi na wananchi kwa jumla waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar sambamba na Serikali za Wilaya kwa mambo yote yanayofanyika katika maeneo yao.

Alifahamisha hatua hiyo itasaidia kuwa  pamoja na malengo waliojipangia hasa katika suala la maendeleo.

“Sisi viongozi wenu tupoa tayari wakati wowote kuisaidia Serikali katika Shughuli zote za maendeleo hivyo nakuombeni nyote mjikubalishe kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ya jimbo na Kitaifa” alisema.