NA MWAJUMA JUMA

MWAKILISHI wa jimbo la Malindi Mohammed Ahmada amesema kuendelea kufanyika mashindano ya vijana, ndio msingi imara wa kupata vipaji vya wachezaji ambao watakuja kusaidia soka la Zanzibar baadae.

Alitoa kauli hiyo  wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mashindano ya vijana ya wilaya ya Mjini Unguja yaliyofanyika huko Amaan.

Alisema hatua hiyo ni nzuri na yeye kama mdau wa michezo ataendelea kuunga mkono juhudi zao, katika kusaidia soka la Zanzibar.

“Nimefarijika sana kwa kukamilisha mashindano hayo na pia kwa kweli tumeona vipaji vya vijana wetu uwanjani”, alisema.

Hata hivyo alichukua fursa hiyo kuzipongeza timu zake za jimbo la Malindi Annour na Weles, ambazo zimefanikiwa kupata ubingwa wa ligi na kombe la Mtoano kwa daraja la Central na Juvenile.

Alisema vijana hao walijitahidi katika ligi zao hizo na kufanikiwa kutimiza malengo yao ambayo kwa kweli ni hatua nzuri ya kujivunia.