NA MWANAHAWA HARUNA SCCM

WATU wawili ambao ni watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika tasisi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi kwa tuhuma za utapeli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji, alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao Agosti 12 mwaka huu.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Biubwa Sudi Mohammed (48) mkaazi wa Mwera ambae ni Mwalimu wa skuli ya Msingi Fuoni Melinne na Haji Ali Amour (45) mkaazi wa Kisauni ambae ni Ofisa Takwimu Idara ya Elimu wilaya ya Mjini.

Alisema watuhumiwa hao wapo watatu ambao mmoja wao alietambulika kwa jina la Ali Khamis Rashid (42) mkaazi wa Tomondo yeye si muajiriwa kwani ameshafukuzwa kazi kwa tuhuma hizo hizo za utapeli.

Aidha alisema watuhumiwa hao wote wanatuhumiwa kwa kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu ambapo Julai mwaka 2020 katika siku tofauti na maeneo tofauti ya Mkoa wa Mjini Magharibi wote kwa pamoja walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa watu 20.

Kamanda Awadh, alisema watuhumiwa hao waliwalangai watu hao kuwasaidia kupata ajira serikalini katika kazi ya ualimu na uhudumu ifikapo mwezi Septemba mwaka jana na kuwataka kila mmoja kutoa kiasi cha pesa shilingi 1,000,000 na kufaikiwa kujipatia fedha hizo isivyo halali jumla ya kiasi cha shilingi 19,000,000.

“Watuhumiwa hawa ilipofika mwezi Septemba mwaka jana waliendelea kuwadanganya kuendea kuwa na subira mpaka litakapomalizika zoezi la uchaguzi mkuu wa Oktoba na baada ya uchaguzi kumalizika wakaendelea kuwalaghai na baadae walibaini kuwa wametapeliwa ndipo walipofika polisi kuripoti,” alibainisha.