NA KHAMISUU ABDALLAH

MWANAMAMA alimdanganya mwenzake kumuuzia kiwanja na kuchukua fedha taslimu shilingi 10,000,000 amepandishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la Fatma Nassor Ali (45) mkaazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mohammed Ali Haji na kusomea na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ghania Mohammed Ali kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 301 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa April 23 mwaka jana majira ya saa 6:15 mchana huko Kiembesamaki wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mshitakiwa huyo kwa lengo la kujipatia shilingi za kitanzania 10,000,000 alimdanganya Said John Nderema kwa kumuuzia kiwanja kilichokuwepo Mfenesini wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wakili Ghania alidai kuwa mshitakiwa huyo aliuza kiwanja hicho wakati akijua kuwa kiwanja hicho sio chake jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mahakama ilisema dhamana ya mshitakiwa huyo ipo wazi ikiwa mshitakiwa huyo atajidhamini mwenyewe kwa shilingi 200,000 fedha taslimu na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha wa Shehia wanazoishi zinazoonesha nambari za nyumba.

Hakimu Mohammed aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Hadi mwandishi wa habari anaondoka mahakamani hapo mshitakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti hayo.