ZASPOTI
MSANII, Rihanna sasa ni bilionea na mwanamuziki tajiri zaidi wa kike duniani, kulingana na Forbes.
Nyota huyo wa ‘pop’ ana thamani ya dola bilioni 1.7 (pauni bilioni 1.2), huku wastani wa dola bilioni 1.4 zikitoka kwa thamani ya kampuni yake ya vipodozi ya Fenty Beauty.
Utajiri wake wote zaidi unatoka kwa kampuni ya mavazi ya ndani , Savage x Fenty, yenye thamani ya dola milioni 270, na mapato yake kutoka kwa muziki na uigizaji.

Yeye ni wa pili baada ya Oprah Winfrey kama mtumbuizaji tajiri wa kike duniani.
Rihanna ambaye jina lake halisi ni Robyn Fenty, alizindua Fenty Beauty mnamo 2017 kwa kushirikiana na kampuni ya bidhaa za kifahari LVMH.
Wakati huo, alisema, lengo kampuni yake hiyo lilikuwa kumvutia ‘kila aina ya mwanamke’ na kuzindua aina 40 za vipodozi , ambavyo wakati huo vilikuwa havijawahi kutokea.

Ilisababisha kile kinachoitwa ‘Athari ya Fenty’ ambapo kampuni nyengine zilipanua safu zao za aina ya bidhaa za vipodozi .
Kampuni hiyo ilileta zaidi ya dola milioni 550 kwa mapato ya kila mwaka katika mwaka wake wa kwanza, LVMH ilisema.
Sio biashara zote za Rihanna zilizolipa, hata hivyo.
Mapema mwaka huu, msanii huyo mwenye umri wa miaka 33 alikubaliana na LVMH kufunga lebo yake ya mitindo ya Fenty baada ya chini ya miaka miwili katika utengenezaji wa nguo za fasheni .

Mwimbaji huyo wa Barbados ameuza zaidi ya rekodi milioni 250, lakini hajatoa albamu ya studio tangu Anti ya 2016.
Lakini, hivi karibuni alionekana akifanya video ya muziki na mpenzi wake, rapa A $ AP Rocky.
Rihanna, ambaye kwa kiasi kikubwa amejiondoa kwenye tasnia ya muziki, amekuwa na miaka mitano tangu albamu yake ya mwisho kutoka na amejikita zaidi katika tasnia zisizo za muziki, licha ya wito wa mashabiki wake kutengeneza nyimbo mpya.(AFP).