NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameeleza kuwa atatumia mchezo dhidi ya Zanaco FC ya Zambia jumapili hii, kuwa kigezo kwa mchezo wake na Rivers United ya Nigeria.

Yanga imepangwa kucheza na Rivers United katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali wa ligi ya mabingwa Afrika unaotarajiwa kupigwa kati ya Septemba 10 na 12, mwaka huu jijini Dar es salam, kabla ya kwenda kumalizia ugenini kati ya Septemba 17 na 19.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya mchezo dhidi ya Rivers United, Nabi alisema alieleza kuwa: “Tumerejea Dar es Salaam baada ya kambi ya muda kule nchini Morocco, lengo lilikuwa ni kujiandaa na mashindano ya msimu mpya,”.

Aliongeza kuwa, “Mbele yetu tuna matukio mawili makubwa ambayo tunajiandaa nayo. Kuna mchezo wa kilele cha wiki ya mwananchi tutakaocheza dhidi ya Zanaco ya Zambia, benchi la ufundi tumejipanga kuutumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi dhidi ya Rivers United,”.