NA TATU MAKAME

NAIBU Spika wa Bazara la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma ameitaka jumuiya ya kiislamamu ya wanawake kuendeleza sherehe za kiislamu na kuzipa kipaumbele, ili vizazi vijavyo vinufaike na sherehe hizo.

Mgeni alisema hayo huko Malandege Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, katika sherehe za kuuaga na kuukaribisha mwaka mpya wa kiislamu 1443.

Alisema ipo haja kwa jumuiya hiyo kuzipa kipaumbele sherehe za kiisalamu kwa manufaa ya vizazi vijavyo katika kuendeleza mambo ya kheri na kuendeleza mambo mema yenye misingi ya dini ya kiislamu.

Alisema kuendelezwa kwa sherehe hizo ni kielelezo cha kuzipa kipaumbele sherehe za kiislamu ambazo zinaachwa nyuma kulinganisha na sherehe nyengine.

“Ukifika mwisho wa mwaka watu wanasherehekea kwa kumuasi Mwenyezi Mungu hivyo ipo haja ya kuendeleza sherehe hizi ili zitambulike kama sherehe nyengine”, alisema.

Naibu huyo, ambae pia ni mlezi wa jumuiya hiyo, aliwataka wanawake hao kukumbushana mambo ya heri yatakayoleta manufaa kwa wanawake katika maslahi yao ya dunia na akhera.

Hata hivyo, aliwasisitiza wanawake kuongeza upendo, mshikamano, na kuleta Amani baina yao na jumuiya hiyo inapaswa kuisambaza dini ya kiislamu kwa kuendeleza kutoa mihadhara na mikusanyiko ya kheri, ili kuipa nguvu dini ya kiislamu.

Nae Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Panya Ali Abdalla aliwasisitiza wanawake kuendeleza kutoa michango ya ujenzi wa msikiti wa Ijitimai ya kimataifa unaoendelea Kidoti, ili kumalizia ujenzi wake kabla ya shughuli za Ijitimai kufika.“Twendeni tukawekeze ile ndio benki yetu kila mmoja aweke amana yake kujenga akhera yake”, alisema.