Wako wanaoendelea kuchanja, wengine wasema kwanza bado

NA HUSNA MOHAMMED

SIKU chache ikiwa wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na watoto Zanzibar ikitaja maeneo ambayo yatatolewa chanjo kwa ajili ya corona watu kadhaa wameonesha hisia zao juu ya chanjo hizo.

Wakizungumza na makala haya kwa nyakati tofauti, wako watu waliofurahia kupata chanjo hiyo na wako waliokataa huku wakitoa sababu mbalimbali.

WATU WALIOONESHA NIA YA KUCHANJA NA WALIOCHANJA

Baadhi ya wananchi walioonesha nia ya kutaka kuchanjwa walisema kwa muda sasa wamekuwa wakifuatilia taarifa juu ya chanjo hizo na kwamba kutolewa kwa chanjo hizo kutawafanya kwenda kuchanja bila ya kulazimishwa.

“Nilikuwa nasubiri kwa hamu kubwa, leo hii nimeenda kituo cha chanjo kusikiliza utaratibu wa chanjo”, alisema Khamis Fakihi mkaazi wa Jumbi.

Nae Hamisa Jumbe Kae mkaazi wa Fuoni, anasema kwa miaka takriban saba anaishi na ugonjwa wa kisukari hivyo anaamini chanjo hio ya corona itamsaidia kujikinga na ugonjwa huo.

“Mimi nilikuwa sijui kama tayari serikali imetangaza chanjo hizo kwa wananchi lakini sasa nishajua nitatafuta njia ya kufika kuchanja”, alisema.

Kwa upande wake Issa Machano Ngwali, ambae ni mchuuzi wa samaki, anasema anaona umuhimu wa kuchanja kwa kuwa hukutana na watu tofauti kwa kazi yake.

Nae Monica Saimon, ambae ni mfanyakazi wa hoteli moja ya kitalii, alisema kuwa aliogopa kupoteza ajira yake kwa kukosa chanjo.

“Hoteli nnayofanyia kazi ni lazima uoneshe kadi ya chanjo ya corona na tulikuwa tushapewa muda, sikujua wapi zinapatikana kwa sababu utaratibu haukuandaliwa kazini, lakini niliposikia tangazo nikaona sasa niende nikachanje”, alisema.

WASIOTAKA KUCHANJA CORONA

Nae Asha Salim Kingali, alisema haoni umuhimu wa kuchanja kwa sasa na kusema ni mapema mno kufanya hivyo.

“Nasubiri kwanza watu waliochanjwa nione matokeo yao halafu na mimi nitachanja lakini kwa sasa sitaki hasa kwa kuwa sina maradhi sugu na afya yangu iko vyema”, alisema.

Nae Ikram Khatibu alisema ingekuwa chanjo ya Johson Johson (JJ) angalichanja kwa kuwa ni mara moja tu kuchanja lakini hii ya Sinovac ni mara mbili hivyo kwa sasa hatochanja.

“Labda nisafiri nje ya nchi na nitaenda Dar kuchanja kwa sababu hii unachanja mara moja tu, lakini hii ya hapa Zanzibar lazima uchanje mara mbili”, alisisitiza.

Mwanamke mwengine wa miaka 31 ambae alitaja jina moja la Nesi, alisema labda Serikali itangaze lazima kuchanja, lakini kwa sasa hajaona ulazima wa kufanya hivyo.

Siendi kuchanja wakati si lazima ni hiari ya mtu, labda serikali itangaze lazima na pia kama nitakosa baadhi ya huduma kwa kutochanja corona ndio nitaenda, lakini kwa sasa sijaweka hata siku ya kuchanja”, alisema.

VIONGOZI WA DINI WANASEMAJE KUHUSINA NA CHANJO

Padri wa Kanisa Anglican Zanzibar, Godwin Emmanuel Masoud, alisema waumini wa kanisa hilo wana maamuzi yao ya kuchanja corona.

“Sisi kama kanisa hatujamkataza wala kumlazimisha muumini kuchanja corona na kwa kuwa ni hiari ya mtu basi kama atafanya anavyotaka sawa”, alisema.

Aidha alisema kuwa kama wao viongozi wa kanisa wanaaminika, bado wanaendelea kutoa taaluma juu ya kinga ya corona na wataendelea kufanya hivyo kusudi kuona hakuna maambukizi kwa waumini wa kanisa hilo.

“Tunaendelea kutoa taaluma na ndio maana tangu wimbi la kwanza tumeweka ndoo za maji ili watu kunawa mikono pamoja na vitakasa mikono na tutaendelea kufanya hivyo kwani dini pia inataka usafi wa mwili na wa kiwiliwili”, alisema Padri huyo.

Nae mmoja wa waumini wa kanisa hilo ambae hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema yeye tayari amepata chanjo ya corona hasa kutokana na kazi yake.

“Mimi ni dereva nawatembeza wageni, nimeona bora nichanje kwa sababu watu ninaowahudumia hasa wageni siwajui wako vipi”, alisema.

Kwa upande wa kiongozi mmoja wa dini ya kiislamu ambae hakutaka kutajwa jina lake gazetini yeye anasema kuwa chanjo hazina madhara yoyote kwa kuwa wazanzibari wameshachanjwa chanjo nyingi na hakuna madhara yaliyoripotiwa.

“Watoto wetu kuanzia kuzaliwa mpaka mwaka mmoja na nusu wanachanja siku zote na chanjo nyengine hadi miaka mitano pia wanachanjwa zinawalinda na magonjwa mengi kwa hivyo hakuna sababu ya kukataa chanjo kwa afya ya mtu”, alisema.

Alifahamisha kuwa kama chanjo zimethibitishwa na wataalamu hakuna sababu ya kupinga na kwa kuwa si lazima basi kila mmoja ana khiari yake.

“Mimi binafsi wakati wowote nitachanja kwa sababu waliochanja sijasikia madhara yake hadi sasa hivyo kama kiongozi wa dini basi anaetaka achanje asietaka basi, lakini kuna baadhi ya mambo yatalazimika mtu achanje kama kusafiri nje ya nchi”.

WAFANYAKAZI WAHUDUMU WA AFYA

Wahudumu wa afya waliopata chanjo ya corona Zanzibar wamewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kuhusina na chanjo hiyo na kusema kuwa ni salama.

Wakizungumza na gazeti hili huko hospitali ya rufaa Mnazi mmoja, walisema kuwa tangu walipochoma chanjo hiyo hakuna madhara wala mabadiliko yoyote waliyoyapata kwenye miili yao na wametumia nafasi hiyo kutaka wananchi itakapokuwa tayari kuchanjwa kujitokeza kwa wingi.

Afisa Muuguzi Mwandamizi wa kitengo cha chanjo ya corona katika hospitali ya Mnazimmoja, Mwanahawa Ngwali Ahmeid, alisema yeye ameshamaliza dozi zote mbili na hakuna tatizo lolote alilopata baada ya kuchanja chanjo hiyo.

“Dozi yangu ya kwanza nimechoma tarehe 13 mwezi huu na ya pili nimeipata jana (juzi) na hakuna tatizo, nimelazimika kuchanja kwa sababu niko katika hatari ya kuweza kupata maambukizi kwa kazi zangu za huduma ya afya”, alisema.

Akizungumzia kuhusiana na muitiko wa wahudumu wa afya waliopata chanjo hiyo, Afisa huyo alisema zaidi ya wahudumu wa afya wapatao 50 wameshapatiwa chanjo hiyo na wengi wao wameshakamilisha dozi ya pili.

Nae Daktari bingwa wa kitengo cha masikio, pua na koo katika hospitali hiyo ya Mnazi mmoja, Dk. Khalid Yussuf Alawi, alisema kwa kuwa chanjo ni hiari amelazimika kuchanja ili kujikinga na ugonjwa wa corona.

Alisema ugonjwa wa corona upo na jamii haipaswi kudharau na kwamba serikali kuleta chanjo hiyo haikukuurupuka ila imeona haja ya kuwalinda raia wake.

“Kama wako wanaopotosha chanjo hawaitendei haki serikali na wao binafsi lakini mimi nimeamua kuchanja na kumaliza dozi zote mbili na hakuna athari yoyote niliyoipata”, alisema.

Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo ya bure kuchanja ili kujikinga na ugonjwa wa corona jambo ambalo litawasaidia sana kuiweka afya yao imara.

Nae Issa Khamis Ali, ambae ni Afisa muuguzi msaidizi, alisema kuwa amemaliza dozi ya chanjo ya corona na hadi sasa yuko sawa.

Alisema kuwa ingawa chanjo ya corona ni hiari, lakini pia jamii haipaswi kupuuza kwa kuwa itawasaidia kujikinga na corona.

WIZARA YA AFYA, USTAWI WA JAMII JINSIA NA WATOTO

Mapema hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na watoto, Nassor Ahmeid Mazrui, alisema kwa sasa Serikali kupitia wizara hiyo imeanza kutoa chanjo ya corona kwa makundi maalumu ambayo ni hatarishi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu ambayo ni pamoja na wafanyakazi wa milango mikuu ya kuingia nchini (Viwanja vya ndege na Bandarini).

 

Aliyataja Makundi mengine ni waongoza watalii, madereva wanaosafirisha wageni na watalii, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri vya ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wa mahoteli, wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu.

ZOEZI LA UTOAJI WA CHANJO ZA CORONA

Waziri huyo alisema chanjo zinazotolewa Zanzibar ni Sinovac na Sputnik Light 5 ambazo zimeanza kutolewa Juni 17, 2021 na hadi kufikia August 10 jumla ya watu 9,350 wameshachanja kati yao 5,447 wamekamilisha dozi na 3,903 wanasubiri kukamilisha dozi zao.

MAENEO HUSIKA YA CHANJO YA CORONA

Mazrui alitaja maeneo chanjo hizo zinapopatikana kuwa ni katika kitengo cha kupambana na kudhibiti maradhi ya miripuko Lumumba na Hospitali ya Mnazi mmoja lakini chanjo hizo zitatolewa hospitali za Kivunge,Makunduchi, Abdalla Mzee, Wete na hospitali ya wilaya Chake Chake.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni Micheweni, kituo cha Afya Tunguu, kituo cha Afya Fuoni na kituo cha Afya Kianga hivyo aliwaomba wananchi kujitokeza kupata chanjo kujenga kinga dhidi ya ugonjwa huo .

“Chanjo zinazotolewa Zanzibar ni salama na zimethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na imeshatumika katika nchi kadhaa duniani na kuleta matokeo chanya,” alieleza Waziri Mazrui.

ELIMU ZAIDI YA CORONA KWA JAMII

Kwa upande wa elimu ya afya kwa jamii, Waziri Mazrui. alisema pamoja na utoaji wa chanjo hiyo bado jamii inatakiwa kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga ugonjwa huo ili kusaidia kupunguza kujikinga na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu hapa nchini.

Aliwasisitiza, kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama inavyoshauriwa na wataalamu na wizara ya Afya ikiwemo kukaa umbali usiopungua mita moja baina ya mtu na mtu, matumizi ya maji salama kwa kukosha mikono au kutumia vitakasa mikono,matumizi ya barakoa,kuepuka kupeana mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.​

Katika hatua nyengine, Waziri Mazrui, alitahadharisha jamii juu ya wimbi la nne la ugoinjwa huo linalojulikana kwa jina la Lamda ambalo limeshaanza katika nchi ya Peru na linashuka katika nchi za Marekani ya Kusini ambalo lina athari zaidi.

CHANJO NYENGINE KUWASILI TENA

Nae Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Abdalla Ali, alisema wizara itatoa muongozo kwa makundi mengine yanayotaka kupata chanjo hiyo mara tu wizara itakapotoa taarifa rasmi na kupokea mzigo mwengine kwani chanjo iliyokuwepo haitoshelezi kwa Zanzibar nzima.

Hata hivyo, alisema chanjo zote zinazopokelewa Zanzibar haijanunua kama serikali bali ni msaada na mzigo mwengine wanaotarajia kuupata ni msaada wa watanzania nzima kwa Tanzania bara na Zanzibar kupitia mpango maalum uliotayarishwa na Umoja wa Mataifa ambayo itapokelewa ndani ya wiki mbili.

UKUBWA WA TATIZO LA CORONA ZANZIBAR

Hadi kufikia wiki iliyopita jumla ya watu 15 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa corona hapa Zanzibar, huku watu 390 wakigundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo wakiwemo Watanzania 112 na wageni 278 kutoka mataifa mbali mbali duniani.

Kati ya watu hao wamo watu 29,326 waliopimwa katika vituo na hospitali mbali mbali Unguja na Pemba kuanzia Juni 25 hadi Agosti 10 mwaka huu.

Aidha watu 390 waliothibitika kuwa na maambuki ya virusi vya Corona, 207 wamepona na wanaendelea na majukumu yao na wagonjwa waliobaki ni 183 (Watanzania 32 na wageni ni 151) na wagonjwa 24 wamelazwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.

NINI UGONJWA WA CORONA

Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Cov) ni familia ya virusi vinavoysababisha ugonjwa kuanzia mafua ya kawaida hadi magonjwa makali zaidi kama vile matatizo ya kupumua (MERS-CoV) na SARS-CoV.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) lilisema kuwa ugonjwa wa virusi vya Corona vya COVID-19 ni mripuko mpya uliogunduliwa mwaka 2019 na havikuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa bindamu.

Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi, shida katika kupumua, na katika hali ngumu zaidi, maambukizi yanaweza kusababisha, nimonia, kukosa pumzi, kushindwa kufanyakazi kwa figo na hata kifo.

Aidha WHO lilisema kuwa hadi kufikia mwezi uliopita wa Julai zaidi ya watu milioni 4 wamefariki kwa ugonjwa wa corona huku watu wapatao milioni 183,934,913 wakiougua ugonjwa huo.