TOKYO, JAPANI

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Japani Motegi Toshimitsu amesisitiza kuwa nchi zinazotoa mikopo zinapaswa kufuata sheria za kimataifa zinapotoa mikopo hiyo kwa ajili ya utekelezaji miradi katika nchi zinazoendelea.

Motegi alitoa maoni hayo wakati wa mkutano uliofanyika mtandaoni wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Japani, China na Korea Kusini.

Alisema mikopo kwa mataifa yanayoendelea huenda ikaongezeka kwani dunia inaendelea kuimarika kutoka kwenye janga la virusi vya korona.

Aidha Motegi alisema utoaji mikopo unapaswa kufanywa katika hali ya usawa na uwazi kuhakikisha uhuru wa nchi zinazokopeshwa na ukuaji endelevu.

Inaonekana maoni yake yalilenga kuhakikisha ufuatiliaji wa mikopo mikubwa inayotolewa na China, na ambayo imeziacha nchi zinazokopeshwa kwenye kile kinachoitwa mtego wa mkopo.