NA SAIDA ISSA, DODOMA
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwakani ili kuiwezesha serikali kupanga maendeleo na kukuza uchumi.
Agizo hilo limetolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachanwene wakati wakichangia katika kikao cha uhamasishaji na utoaji wa elimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Spika Ndugai ambaye ni mbunge wa alisema zoezi hilo ni muhimu kwa Taifa kwani litasaidia nchi kupanga maendeleo hivyo watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.
“Tarehe 31 vikao vyetu vya Bunge vitaanza na vikao vilivyopita tumepitisha mambo mengi ikiwemo na tozo, safari hii itakuwa salama. Hili ni jambo muhimu sana hivyo niwaombe watanzania wajitokeze kwa wingi,sisi wagogo hata zoezi la kuhesabu mifugo linakuwa na shida ni utamaduni wetu,”alisema.
Kwa upande wake, waziri Simbachawene alimpongeza mkuu wa mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka kwa kuandaa mkutano huo huku akisisitiza kwamba sensa ni muhimu kwani inaleta ushahidi wa kisayansi na maendeleo.
Naye Kamisaa wa Sensa nchini ambaye pia ni Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda ametoa wito kwa watanzania kujitokeza katika zoezi la kuhesabiwa kwani hilo sio suala la kisiasa.
Alisema katika zoezi hilo watatumia tehama katika maeneo ya kuhesabiwa lengo likiwa ni kuwafikia watanzania wengi ambapo amedai watawafikia watu wengi mpaka katika maeneo ya vijijini.
Makinda alisema wamejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi kwani kwa sasa wataaalamu wameongezeka tofauti na miaka ya nyuma.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa alisema serikali imejipanga kikamilifu kusimamia zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani huku akitoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi hilo.
“Sensa hii itakuwa ni ya sita itasimamiwa na Serikali ya awamu ya sita kwa weledi mkubwa tunatarajia watahesabiwa zaidi ya watu milioni 64 kwani kila mwaka watu wanaongezeka milioni 3.1 na sensa mwisho ya mwaka 2012 tulikuwa milioni 49,”alisema.