NASRA MANZI NA ABOUD MAHMOUD
MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa ameitaka timu ya soka ya Wanawake ya ‘New Generation Gueens’ kujituma ili kujitengenezea soko la ajira.
Akizungumza na wanamichezo hao katika hafla ya kuwaaga pamoja na kuwakabidhi Bendera ya Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kombe la klabu Bingwa Afrika Mashariki katika Ofisi zake zilizopo Vuga Mkoa wa Mjini.
Alisema endapo watacheza mpira kwa malengo itapelekea kupata wafadhili na kupata kujiuza kimichezo na kucheza mpira nchi za nje.
Amewataka wanamichezo hao kwenda kushindana na sio kushiriki kwa lengo la kuiwakilisha Zanzibar na kurudi na ubingwa ,sambamba na kufanya kazi kwa mashirikiano na kuondosha tofauti zao.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab alisema ni vyema vijana kudumisha nidhamu,mila ,kulinda utamaduni kwa ajili ya kwenda kupambana na kuipatia sifa nchi kimichezo.
Nae Kamishna Idara ya michezo Zanzibar Ameir Mohammed Makame amewataka wachezaji kwenda kushindana kwa ajili ya kuweka alama Zanzibar katika michezo.
Mwenyekiti wa timu ya mpira wa miguu Wanawake New Generation queens Farid Mohammed Hamza ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwawekea mazingira mazuri wanamichezo pamoja na sera zilizo rafiki.
Kwa upande wake msemaje wa New Generation,Ismail Ali Juma alisema kikosi hicho kimeondoka nchini kikiwa na wachezaji 23 na viongozi saba.
Wawakilishi hao ambao wameondoka jana Zanzibar ambapo leo wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kuelekea jijini Nairobi nchini Kenya.