NA SABRA MAKAME, SCCM

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid ameipongeza benki ya NMB kwa misaada mbali mbali wanayotoa kwa jamii hapa Zanzibar.

Alisema wananchi wa maeneo mbali mbali wamekuwa wakilalamikia changamoto za kijamii, ikiwemo sekta ya elimu kukosekana kwa madarasa ya kusomea baadhi ya madarasa kuvujisha hivyo msaada uliotolewa na benki hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha changamoto hizo.

Rashid alieleza hayo juzi wakati akipokea vifaa vya kuezekea skuli za mkoa huo na vitanda kwa ajili ya kujifungulia mama wajawazito ili kuwasaidia kwa namna moja ama nyengine.

Alisema msaada huo una thamani ya shilingi milioni 25 utatumika kuezekea skuli tatu kwa mkoa huo ikiwemo ya Kizimkazi, Makunduchi na Binguni.

“Serikali ya Mapinduzi imekua ikithamini na kutambua misaada inayotolewa na wadau wa maendeleo kama benki ya NMB kwani imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za wananchi wetu,” alieleza Mkuu huyo wa mkoa.

Aidha Rashid aliipongeza benki hiyo kwa kuwa karibu na serikali na kuwasaidia wananchi wa Zanzibar wakiwemo wakulima wa mwani na wavuvi kwa kuzingatia sera ya Rais wa Zanzibar kuiendeleza sekta ya uchumi wa buluu.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika skuli ya Binguni, NMB pia ilikabidhi vitanda 12 kwa ajili ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za mama na watoto vya sehemu mbali mbali kikiwemo cha Mwera, Chwaka na Unguja Ukuu.

Aidha aliwaomba wananchi wa mkoa huo kutumia vyema haduma  inayotolewa na benki hiyo kuhusiana na programu inayojulikana wajibu ambapo inawafahamisha wanafunzi jinsi gani watumie na watunze fedha.

Rashid aliziomba taasisi nyengine kuiga mfano wa NMB na kutoa misaada mbali mbali itakayowanufaisha wananchi kutatua changamoto za maji, barabara na masoko ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wake, Ofisa  Mkuu wa  Wateja binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, alisema NMB imetoa msaada huo kama sehemu ya utaratibu wa benki hiyo kutenga  asilimia ya faida inayoipata kurejesha kwa wananchi.