NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

BENKI NMB imeendelea kuongoza kwenye vigezo vya ufanisi kiutendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2021 nchini Tanzania ikilinganishwa na taasisi nyengine za kifedha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna (pichani), imeonesha kuwa faida baada ya kodi ya mapato imeongezeka kwa asilimia 43 na kufikia shilingi bilioni 134 ikilinganishwa na shilingi bilioni 94 ya kipindi kilichoishia mwezi Juni 2020.

Aidha zaipuna alieleza katika taarifa hiyo kuwa ufanisi huo umetokana na ongezeko la biashara na miamala, udhibiti wa gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo inayotolewa.

“Mapato ya Benki yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia shilingi bilioni 463 katika kipindi kilichomalizikia mwezi Juni 2021 ikilinganishwa na shilingi bilioni 387 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana,” alieleza Mtendaji huyo.

Alifafanua kwamba ongezeko la mapato limechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za serikali wakati mapato yasiyotokana na riba yameongezeka kwa asilimia 17 na kufikia shilingi bilioni 140 ikilinganishwa na shilingi 119 ya kipindi kama hicho katika mwaka 2020.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, uwiano wa matumizi yasiyo ya riba na mapato halisi umeimarika mpaka asilimia 47, kutoka asilimia 56 katika kipindi kama hiki mwaka uliopita ambao umo ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 55 ya kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Alifafanua kwamba, katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka 2021, ubora wa mali za benki hiyo umeimarika kutokana na mikakati ya kuimarisha mikopo ya benki lakini pia uwiano wa mikopo chechefu umeimarika hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 6.9 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mizania yake ikiwa na ukuaji endelevu hivyo kuonesha kwa jinsi gani benki imeweka misingi bora na imara ya uhusiano wake na wateja.