NAIROBI, KENYA

KENYA huenda ikaingia kwenye wimbi la nne la maambukizi ya virusi vya Corona ambalo lilitabiriwa mapema na wataalamu wa magonjwa, wakati ambapo mji mkuu Nairobi na kaunti nyengine nane zikishuhudia idadi ya wagonjwa na vifo ikiongezeka sana.

Wizara ya Afya ya Kenya ilisema idadi inayoongezeka ya wagonjwa wa UVIKO-19, kwa kiasi kikubwa inachangiwa na virusi vya Delta na kuregeza hatua za kudhibiti ugonjwa huo, na huenda ikasababisha wimbi la nne.

Kwenye mkutano uliofanyika Julai 30 mjini Nairobi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kupanda ghafla kwa idadi ya watu wanaogunduliwa kuwa na virusi vya Corona baada ya kutulia kwa muda, kunaweza kurejesha nyuma hatua za kushusha idadi hiyo.

Alifafanua kuwa vituo vya afya mjini Nairobi vimezidiwa kutokana na ongezeko la wagonjwa, na kwamba mahitaji ya oksijeni yamekuwa makubwa wakati ambapo wagonjwa wenye dalili ndogo wamekuwa wakizidiwa kwa kasi kubwa.