NA MWANDISHI WETU, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuna umuhimu kwa watendaji wa sensa kuwafikia viongozi wa vyama vya siasa ili kuwafikishia kwa usahihi wananchi umuhimu wa sensa ya watu na makaazi.

Makamu huyo alieleza hayo jana ofisini kwake Migombani alipokutana na kufanya mazungumzo na kamisaa wa Sensa ya Watu na Makaazi Zanzibar, Balozi Mohammed Haji Hamza na watendaji wa Ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia wananchi kupata elimu sahihi juu ya sensa ya watu na makaazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwakani ambapo viongozi hao watasaidia kuwafahamisha wananchi umuhimu wa sensa na kusaidia kuepuka uelewa mbaya kuhusu sensa.

Alisema ni vyema wananchi wakaelimishwa ili wafahamu kwamba kushiriki katika sensa ni uwekezaji muhimu katika upangani na uwekaji wa mipango sahihi ya maendeleo ya nchi.

Naye Kamisaa wa sensa Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza amemueleza Makamu huyo kwamba maandalizi ya sensa hiyo yanaendelea ikiwa ni pamoja ukataji wa maeneo ya kuhesabu watu.

Balozi Hamza alifahamisha sensa ijayo itafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuwezesha kukusanywa kwa usahihi takwimu mbali mbali zinazohusu idadi ya watu, makaazi, shughuli za kijamii na mambo mengine mbali mbali.

Katika hatua nyengine hapo jana, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Massoud Othman alikutana na uongozi wa Chama cha Mabaharia Zanzibar na kuahidi kushirikiana na chama hicho katika kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili mabaharia wa Zanzibar.