NA MWANDISHI WETU, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema serikali imedhamiria kuleta mageuzi katika maendeleo ya makaazi, biashara na uendelezaji ardhi ili kiwe kichocheo cha ukuaji wa uchumi Zanzibar.
Othman aliyasema hayo jana alipofungua kongamano na mkutano wa pili wa taasisi ya wataalam wa milki kuu Tanzania huko katika hoteli ya Verde iliyopo Mtoni mjini Zanzibar.
Alisema kwamba migogoro ya ardhi iliyopo bado ni kitendawili na ni tatizo kubwa linalohitaji juhudi za kupatiwa ufumbuzi wa haraka na kwamba wataalamu wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kupatikana suluhisho sahihi la tatizo hilo.
Alisema kongamano hilo linalowakutanisha wataalamu wa masuala ya ardhi, uwekezaji, wathamini wa majengo na maafisa ardhi litasaidia kujadili na kutafuta njia muafaka za matatizo ya ardhi ili kuifikiasha Tanzania katika uchumi bora kupitia tasnia hiyo.
Aliongeza kwamba iwapo suluhisho la migogoro ya ardhi litapatikana wananchi watatekeleza ipasavyo majukumu yao ya kilimo, ufugaji na ujenzi kwa tija zaidi kuliko ilivyo sasa.
Alifahamisha kwamba hivi karibuni serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mabadiliko katika sheria ya kukuza na kuendeleza uwekezaji Zanzibar, ambayo yanalenga kufungua furasa zaidi za uwekezaji kwa upande wa kisiwa cha Pemba kwa nia ya kukuza uchumi na maendeleo.
Makamu aliongeza kwamba mabadiliko hayo ya kisheria pia yamelenga kuongeza fursa na vivutio vipya vya uwekezaji wa biashara ya majengo na wanunuzi wa nyumba zilizoko katika miradi ya uwekezaji Unguja na Pemba.
Aliwakumbusha wataalamu wa mipango miji kuelewa kwamba nchi imevurugika sana kwenye eneo hilo, kwani ipo mitaa mingi ambapo maumbile yake yengekuwa ya kuvutioa sana na yenye haiba na thamani kubwa lakini kukosekana ama kutosimamiwa mipango miji ipasavyo imefanya miataa hiyo kuwa duni na isiyo na thamani.
“Ninaamini mipango miji na usimamizi wake ni moja ya mambo muhimu sana katika kubadili, sio tu haiba bali pia thamani ya ardhi na Majengo. Miapngo miji na bora na usimamizi wenye ufanisi ungefanya mabaraza yetu ya miji kuwa na mapato ya kutosha kutekeleza kazi zao”, alisisitiza.