NA MWANDISHI WETU, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema serikali ipo katika mpango wa kuisimamia biashara ya karafuu ili kuleta tija kwa serikali na wakulima wa zao hilo.

Aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya mikarafuu yaliyopo Kichunjuu, mkoa wa Kusini na Mgogoni, mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa lengo la kusikiliza matatizo yanayowakabili wakulima wa zao hilo.

Othman alisema kwa muda mrefu zao la karafuu limepoteza uhalisia wake katika uzalishaji, jambo ambalo kwa kiasi limekuwa likiwarudisha nyuma wakulima katika kujinyanyua kiuchumi.

“Awali Zanzibar ilikuwa ikizalisha hadi kufikia kilo 20,000 za karafuu lakini sasa wakulima wamekuwa wakizalisha wastani wa kilo 6,000 tu. Mabadiliko yanayotokana na kukosekana kwa miundombinu bora kwa wakulima na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya karafuu inayofika katika soko la dunia,” alifafanua Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Akigusia juu ya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Othman alisema bado kumekuwa na matatizo mengi likiwemo la utoaji wa miche ya mikarafuu ambayo bado haiwanufaishi wakulima kuliendeleza zao hilo.

Hata hivyo, aliwahakikishia wakulima kuwa Serikali itaendelea kuwatatulia matatizo yanayowakabili kupitia mpango ambao utakuza zaidi biashara ya karafuu na kukuza soko lake duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, alisema ili kuhakikisha uzalishaji wa karafuu unakuwa katika kiwango bora, Wizara hiyo ina mpango wa kukutana na wadau wa karafuu kwa lengo la kuandaa muelekeo mpya wa kisera na mageuzi katika uendelezaji wa zao hilo.

“Kutokana na mabadiliko ya soko la karafuu, serikali inaendelea kupanga bei ambazo zitakuwa ni mkombozi kwa wakulima pamoja na kuandaa mazingira rafiki kwa lengo la kukuza uzalishaji wake nchini,” alifafanua Shaaban.

Akizungumzia sifa ya karafuu, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan, alieleza kuwa kutunza ubora wa karafuu hizo limekuwa tatizo kubwa kwa wakulima.

Alisema Wizara kwa kushirikiana na wakulima inaangalia namna ya kuliweka sawa jambo hilo kwa lengo la kuona tatizo hilo linaondoka na wanafaidika.

Aidha alisema Serikali ina mpango wa kuwapa mashamba wakulima hao ambapo kwa sasa Wizara ya Ardhi na maendeleo ya makaazi inaendelea na zoezi la upimaji wa ardhi kwa ajili ya ugawaji huo.

Nao wakulima hao wameiomba serikali kuwatatulia matatizo wanayokabiliana nayo ikiwemo suala la bei ya karafuu, miche pamoja na uharakishaji wa malipo wakati wanapofanya mauzo yao.