NA SABIHAS KEISS- WAMM

WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe Juma, amewapongeza wanakijiji wa Kizimkazi kwa kuungana pamoja na kuanzisha tamasha la watu wa Kizimkazi katika kulinda mila na desturi zao.

Pongezi hizo alizitoa huko Kizimkazi Mkunguni alipokua akizungumza na wanakijiji hao, mara baada ya kumaliza mechi ya mpira wa nage na kuvuta kamba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za siku za ‘Kizimkazi day’.

Alieleza kuwa kushirikiana pamoja na kuanzisha tamasha ni jambo la kupigiwa mfano kwani imeweza kuibua hamasa katika jamii na maendeleo yanaweza kupatikana kupitia tamasha hilo.

Aidha Riziki amezitaka shehia ambazo hazijaungana waige mfano wa watu huo katika kuona kuwa mila na desturi za wazanzibari zinaendelezwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Akizungumzia tatizo la udhalilishaji Pembe ameviomba vyombo vya ulinzi ikiwemo jeshi la polisi na mahakama ,kusimamia ipasavyo sheria zilizoweka ili kuvitokomeza, sambamba na kuitaka jamii kutoa taarifa mara tu vinapotokea vitendo hivi na kuachana  na tabia ya kuonea muhali.

Mapema akisoma risali mjumbe wa kamati ya tamasha la Kizimkazi, Rehema Kassim Ramadhan, alisema kwa sasa changamoto nyingi zimepatiwa ufumbuzi, ambapo azma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika tamasha hilo ni kutanua wigo wa sherehe hizo ambapo lengo ni kuleta maendeleo katika kijiji cha Kizimkazi na tamasha hilo kujulikana kimataifa .