MAPAMBANO DAWA ZA KULEVYA
NA MADINA ISSA
JESHI la Polisi Zanzibar, litafanya operesheni maalum ya kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya katika mikoa ya Tanzania iliyo kwenye ukanda wa mwambao wa pwani ya bahari ya hindi.
Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Mohamed Haji Hassan, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao kilichojadili Mipango ya operesheni hiyo kilichowashirikisha maofisa wa jeshi hilo kutoka Zanzibar na Tanzania bara.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya jeshi hilo yaliyopo Ziwani mjini Zanzibar, pia kiliwashirikisha makamanda polisi wa mikoa iliyo kwenye ukanda wa bahari ya hindi.
Alisema operesheni hiyo imepewa jina la ‘nyangumi’ kutokana na umuhimu wake ambapo itawashirikisha watu mbalimbali wakiwemo watendaji wa jeshi hilo pamoja na wananchi.
Alisema lengo la kikao hicho ni kupanga mikakati ambayo itahakikisha inatekelezwa katika kudhibiti dawa za kulevya hasa kwenye maeneo ya ukanda wa bahari.
Alisema jeshi limeona ipo haja ya kupambana na dawa za kulevya na kufanya uperesheni ya pamoja kwa sababu dawa hizo zikiingia katika mkoa mmoja kati ya mikoa hiyo itakuwa ni rahisi kwenda mkoa mwengine.
“Dawa za kulevya zinazoingia katika mkoa mmoja uliopo baharini athari zinaweza kupatikana katika sehemu nyengine za mwambao wa bahari, hivyo tumeona ni vyema kulidhibiti suala hili ili kuondosha athari”, alisema.
Alisema, uingiaji wa dawa za kulevya umekuwa ukidhoofisha nguvu kazi ya taifa kutokana hasa ikizingatiwa kuwa watumiaji wengi ni rika la vijana ambao ni tegemezi katika uzalishaji wa nchi.
Hivyo, alisema jeshi hilo limepanga kudhibiti maeneo yote ya usafiri ikiwemo bandari na viwanja vya ndege na kusema atakaebainika na kufanya shughuli hizo hatua stahiki zitachukuliwa.
Aidha alifahamisha kuwa, makamanda waliokuwepo katika operesheni hiyo wana uhusiano wa karibu na kushirikiana pamoja katika kudhibiti makosa hayo ya uingizaji wa dawa za kulevya ambapo wasafirishaji wanazitoa sehemu moja hadi nyengine.