NA ASYA HASSAN
JESHI la Polisi la Mkoa wa Kusini Unguja, limeanza kufanya uchunguzi wa majina yaliyofikishwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanaodaiwa kujihusisha na vitendo mbali mbali vya kihalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, ameyasema alipokutana na wakaazi wa shehia nne za jimbo la Uzini kwa ajili yakusikiliza kero zinazowakabili shehia nne ikiwemo Miwani, Ghana, Kiboje Mkwajuni na Mwembe shauri.
Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya Uhalifu katika Mkoa huo na endapo watu hao wakibainika kwa hatua moja ama nyengine wanajihusisha kwa namna yeyote ya kihalifu hatua za kisheria zitachukuliwa zidi yao.
Alisema kukithiri kwa vitendo hivyo ndani ya shehia hizo kumepelekea kuwepo kwa malalamiko na kushindwa kufanya shughuli zao mbali mbali za kiuchumi na kuchangia kurudisha nyuma jitihada zao za kimaendeleo.
Alisema hiyo ni kutokana na kuwapo kwa taarifa za baadhi ya wananchi wa Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Unguja, wanajihusisha na vitendo viovu, ambao vikiendelea kufumbiwa macho vinaweza kusababisha kuleta athari kubwa ndani ya jimbo hilo na vijiji jirani.
Baadhi ya wananchi wanaoishi ndani ya jimbo hilo wamesema, wamekuwa wakijihusisha na vitendo viovu ikiwemo masuala ya udhalilishaji, utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya, wizi wa mazao endapo watu hao wakiendelea kuachiwa wanaweza kusababisha kutokezea kwa athari kubwa ndani ya jimbo hilo.
Wakizitaja miongoni mwa athari zinazojitokeza walisema ni pamoja na wananchi kuendelea kuwa maskini, pamoja na kuwakosa vijana imara watakao weza kusimama kutetea na kulipatia maendeleo taifa lao.
“Kukithiri kwa vitendo hivyo katika maeneo yetu kunatokana na wananchi kutokuwa tayari kuwafichuwa wahalifu wanaofanya vitendo hivyo na kuiyomba serekali kuingilia kati suala hilo, ili vitendo hivyo viweze kupunguwa,”walisema.