LUSAKA, ZAMBIA

RAIS wa Zambia aliyechaguliwa hivi karibuni Hakainde Hichilema ameteua wakuu wapya wa jeshi na kuwabadilisha makamishna wote wa polisi baada ya kuahidi kukomesha ukatili wa polisi uliokuwa ukifanywa wakati wa utawala uliopita.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yalimlaumu rais wa zamani Edgar Lungu kwa kuukandamiza upinzani nchini humo, huku ukatili wa polisi ukitajwa kusababisha vifo vya watu watano tangu aingie madarakani mwaka 2016.

Hichilema,aliwahi kukamatwa mara kadhaa wakati akiwa katika shughuli zake za kisiasa na aliahidi kulishughulikia tatizo hilo katika kampeni zake za uchaguzi.

Wakati wa uteuzi huo, Hichilema aliwasisitiza polisi kwamba hakuna mtu anayepaswa kukamatwa kabla ya uchunguzi kukamilika.