TURIN, Italia
MSHAMBULIAJI nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo ameomba kuachana na klabu hiyo huku akitaka kuuzwa katika majira haya ya kiangazi.
Juventus inasubiri ofa rasmi kutoka katika klabu ya Manchester City, huku ikitarajiwa kufika saa chache zijazo wataafikia makubaliano haraka iwezekanavyo.
Taarifa pia zinasema, wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes anafanya kazi moja kwa moja na bodi ya ManCity kukamilisha makubaliano ya sheria na kataba wa kibinafsi wa Ronaldo.
ManCity pia inataka kuuza baadhi ya wachezaji ili kupata ada ya kumsajili, Ronaldo huku Juventus ikitaka euro milioni 28 hadi 30. Winga Raheem Sterling anaweza kuondoka Man City ikiwa dau wanalolitaka likifikiwa.
Lakini, mshambuliaji, Gabriel Jesus atabakia na meneja, Pep Guardiola anataka kusalia na raia huyo wa Brazil katika msimu huu wa joto.
Wakati huo huo, Real Madrid wamemkomalia mshambuliaji wa Paris Saint Germain, Kylian Mbappe baada ya klabu yake kukataa dau la mwanzo la pauni milioni 130.
Madrid wamerudi tena baada ya maneno ya kejeli ya rais wa PSG kuhusu ofa waliopeleka kwa mshambuliaji wao hatari na kudai klabu hiyo inawajaribu na wanadharau kwa kiwango walichoweka.
Sasa Real Madrid wameweka ofa ya pili kumnasa mshambuliaji huyo kiasi cha pauni milioni 170, wakiwa wameongeza kiasi cha pauni milioni 40 kutoka kwenye ofa ya kwanza.
Kulingangana na ripoti ya Le Parisien, PSG inataka kiasi cha pauni milioni 188 hadi 259 kumuachia, Mbappe, kuondoka.Real inajaribu kusajili mshambuliaji huyo wa Ufaransa zikiwa zimebakia siku chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa, lakini, miamba hiyo ya ‘Ligue 1’ imegoma kumuachia kwa fedha ndogo. (AFP).