KIGALI, RWANDA

WAKILI Mbelgiji wa mwanaharakati wa Rwanda, Paul Rusesabagina, amefukuzwa nchini Rwanda kwa tuhuma za kukiuka sheria ya uhamiaji ya nchi hiyo.

Wakili huyo Vincent Lurquin aliamuliwa kufunga virago  Jumamosi, siku moja baada ya mahakama ya Rwanda kuahirisha hukumu dhidi ya Rusesabagina, ambaye serikali ya Rwanda inamtuhumu kuunga mkono ugaidi.

Mkurugenzi mkuu wa idara ya uhamiaji ya Rwanda, Regis Gatarayiha alisema Lurquin aliingia nchini Rwanda kwa kutumia viza ya watalii, lakini Ijumaa iliyopita alionekana mahakamani, akiwa katika timu ya utetezi ya Paul Rusesabagina, akivalia sare ya kazi.

Gatarayiha alisema wakili huyo hatoruhusiwa tena kukanyaga kwenye ardhi ya Rwanda.

Rusesabagina alipata umaarufu duniani kama shujaa wa filamu ya Hollywood ya ”Hotel Rwanda” kutokana na mchango wake katika kuwanusuru Watutsi zaidi ya 1200 wakati wa mauaji ya kimbari yaliyokuwa yakiwalenga mwaka 1994 nchini Rwanda.Waendesha mashitaka wanataka apewe kifungo cha maisha jela.