NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

HUKUMU ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya anayekabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha akiwa na wenziwe wawili inatarajiwa kutolewa Oktoba 1 mwaka huu.

Sabaya na wenziwe wawili Silvester Nyegu na Daniel Mbura, wamebainika kuwa wana kesi ya kujibu, ambapo ushahidi katika kesi hiyo umekamilika rasmi hapo jana.

Hakimu mkaazi mwandamizi wa mahakama jijini Arusha, Odira Amworo aliwaagiza mawakili wa pande zote kuhakikisha ifikapo Septemba mosi mwaka huu wawe wamewasilisha majumuisho ya mwenendo wa kesi ili mahakama itekeleze jukumu la kutoa hukumu.

Kwa upande wake, wakili wa serikali mkuu Tumaini Kweka aliiomba mahakama hiyo kufanya majumuisho kwa njia ya maandishi ndani ya wiki moja. “Tunaomba siku saba kwa ajili ya kuwasilisha majumuisho kuanzia leo (jana) hadi tarehe mosi mwezi Septemba tuwe tumekamilisha”, alisema Kweka.

Naye wakili kiongozi upande wa utetezi, Dancan Oola alisema watahakikisha wanaleta maelezo yao ifikapo tarehe iliyopangwa 1/9/2021 na wapo tayari kupokea tarehe ya hukumu.

Baada ya maelezo hayo mawakili, hakimu Amworo alieleza mahakamani hapo kuwa shauri hilo litatolewa hukumu rasmi Oktoba 1 mwaka huu.

Awali washitakiwa Lengai Ole Sabaya, Silvester Nyegu na Daniel Mbura kwa pamoja mahakamani hapo walisomewa mashtaka matatu yakiwemo ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kupora mali na fedha tukio ambalo walilifanya Julai 16 mwaka huu.

Kabla ya kukamilika kwa kesi hiyo mshitakiwa wa tatu, Daniel Laurent Mbura (38), aliwahi kueleza mahakamani hapo kuwa hamtambui mshitakiwa wa kwanza wala wa pili katika shauri hilo na alifahamiana nao walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 4 mwaka huu.

Akijitetea mbele ya hakimu Amworo shahidi huyo pia amekanusha majina yaliyopo kwenye hati ya mashitaka ambayo yanasomeka kama Daniel Gabriel Mbura wakati yeye jina lake ni Daniel Laurent Mbura.

Nje ya mahakama wakili wa serikali mkuu Tumaini Kweka alisema kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Julai 16 mwaka huu na imechukua takribani siku 35 kumalizika na wao kama waendesha mashtaka wamekamilisha vyema na wanaiachia mahakama itoe hukumu.

Naye wakili kiongozi upande wa utetezi, Dancan Oola alisema kuwa wao kama mawakili walikuwa sita wakiwatetea washtakiwa watatu ambapo mshtakiwa wa kwanza Lengai Ole Sabaya alitetewa na Dancan Oola na Mosses Mahuna.

Alisema mshtakiwa wa pili Silvester Nyegu alitetewa na mawakili Edmond Ngemela na Silvester Kahunduka huku mshtakiwa wa tatu alikuwa akitetewa na wakili Fridorin Gwemelo na Justine Juston na kwamba wamejipanga ndani ya wiki moja kuwasilisha majumuisho ya mwenendo wa kesi na kusubiri uamuzi wa mahakama.