NA MWANDISHI WETU

JITIHADA za vijana wa Azam FC waliokuwa wanaonolewa na kocha msaidizi, Vivier Bahati kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Kagame, ziligonga mwamba juzi Agosti 11.

Ni katika mchezo wa nusu fainali iliyochezwaUwanja wa Azam Complex, dakika 90 za awali zilimalizika kwa Azam FC na Big Bullets kutoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Bao la mapema la Bright Muthalk dakika ya kwanza liliwapoteza wawakilishi wa Tanzania, Azam FC waliokubali kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao hilo.

Kipindi cha pili waliamka Azam FC na kutengeneza majaribio kadhaa na iliwabidi wasubiri mpaka dakika ya 67 kupachika bao la kusawazisha kupitia kwa Paul Peter.

Kasi ilizidi kuwa kubwa kwa vijana hao ambapo dakika ya 74 nyota wao mwingine Oscar Masai alipachika bao la pili kwa Azam FC.

Bao hilo lilidumu kwa dakika mbili pekee, baada ya makosa ya safu ya ulinzi yalimpa manufaa Bright tena, akapachika bao la kusawazisha dakika ya 76.

Zilipoongezewa dakika 30 hakukuwa na mbabe na Azam FC ilitolewa katika changamoto ya penalti, ambapo ilifunga 2-4 Big Bullets ambao watacheza fainali Jumamosi na Express ambao waliwatoa KMKM.

Bahati alisema vijana wake walipambana kusaka ushindi ila makosa ya kipindi cha kwanza yaliwagharimu na kuwafanya washindwe kushinda mchezo huo.