NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa jeshi la Polisi, familia za askari watatu na familia ya askari mmoja wa kampuni ya SGA waliopoteza maisha jana kutokana na shambulizi la silaha katika eneo la Salenda jijini Dar es Salaam.
Samia ametoa salamu hizo jana kwa kutumia mtandao wake wa twita kufuatia mtu mmoja mwenye silaha aliyejulikana kwa jina moja la Said kuwaua kwa kuwafyatulia risasi askari katika maeneo karibu na Ubalozi wa Ufaransa, Dar es Salaam.
Katika salamu hizo Samia alisema mtu huyo aliyefanya shambulizi hilo amedhibitiwa na hali iko shuwari huku akiliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina.
Katika hatua nyengine mtu huyo aliyefanya shambulizi alisababisha taharuki kubwa katika barabara hiyo eneo la daraja la Salenda, ambapo awali alifyatua risasi hewani akiwa na kipaza sauti kabla ya kuwalenga askari hao.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa tano mchana, na kuwafanya wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo kukimbizana huku na kule ili kujaribu kuokoa maisha yao.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo, ambapo askari wawili na mtuhumiwa huyo wamefariki kufutilia majimbizano ya risasi, ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa na silaha aina ya SMG.
Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuweza kutoa taarifa kamili kwa watanzania.
Mashuhuda mbali mbali waliokuwepo katika eneo la tukio walisema walisikia milio ya risasi, ikilia na watu kuanza kukimbizana na wengine kurudi nyuma ili kuweza kujiokoa maisha yao.
Walisema waliwaona maskari wanakuja kwa ‘speed’ kubwa katika eneo la tukio lililopigwa risasi hizo, ambapo mara waliowana askari wawili na mtu aliyekuwa anafyatua risasi wamefariki hapo hapo.