Ataka wapewe fursa, wawezeshwe

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewahimiza viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuchukua jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake ili wakamate nafasi za uongozi zenye uwezo wa kutoa maamuzi katika nchi zao.

Samia alieleza hayo jana mjini Lilongwe nchini Malawi kwenye mkutano wa 41 uliowakutanisha wakuu wa mataifa na serikali za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC.

Alisema viongozi wa nchi za SADC wachukue fursa ya kuwapa nafasi za uongozi wanawake katika nchi zao na wawasaidie kuwapa msukumo ili wajiamini zaidi katika nafasi walizopewa.

“Na hapa nataka kuwasihi kaka zangu wa ukanda huu wa SADC tuendelee na kushirikiana katika jitihada za kuwainua kiuchumi na kisiasa wanawake katika nchi zetu”, alisema Samia.

Alifahamisha kuwa katika mkutano uliofanyika hivi karibuni wa generation equality uliofanyika nchini Ufaransa ulimchagua kuwa kinara wa masuala ya haki za kiuchumi za wanawake, hivyo aliomba ushirikiano ili yeye na timu yake watekeleze vyema majukumu yao.

Alisema Malawi ni taifa la kwanza la kuwa na Rais Mwanamke, hivyo basi inamaanisha kuongeza msukomo kwa wanawake kujiamini na kuhamasika kuongezeka katika vyombo vya kufanya maamuzi.

Alisema jumuiya hiyo imetoka mbali na imepitia katika matatizo mbalimbali na mwaka jana ilitimiza miaka 40 tangu kuasisiwa ambapo katika kipindi hicho yapo mafanikio mengi yaliyopatikana.

Alisema licha ya nchi hizi kuwa ziko huru, pia kuna ongezeko la wanachama kutoka saba hadi 16, huku ukanda wa Jumuiya hiyo ukiwa bado unasifika kwa kuwepo kwa hali ya amani na utulivu barani Afrika, ingawa kunajitokeza migogoro michache inayojitokeza ambayo inashughulikiwa.

Alisema nchi hizo zinatekeleza vyema demokrasia kwa kuendeleza utaratibu wa kubadilishana uongozi kwani unazidi kushamiri, na mfano mzuri uliojitokeza katika taifa la Zambia, ambao uchaguzi umemalizika na viongozi wa taifa hilo wanakwenda kupokezana majukumu katika hali ya amani.

Akizungumzia suala la ukuwaji wa uchumi, utulivu wa bei, na mifumko ya kukuwa kwa biashara katika mataifa hayo, alisema bado hawapaswi kuridhika na mafanikio yaliyopatikana kutokana na kuwapo mambo mbali mbali yanayoikabili dunia yakiwemo mabadiliko ya tabianchi.

Alisema Tanzania itaendelea kuwa mwanachama muadilifu kwani ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki kuasisi Jumuiya hiyo.

Akizungumzia makabiliano dhidi ya ugonjwa wa corona, Samia alisema lengo la serikali ya Tanzania ni kuhakikisha wananchi wote wanachanjwa ili kupata kinga ya ugonjwa huo.

Aliziomba nchi za SADC kushawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia vibali vya teknolojia zao zitumike ili kuruhusu chanjo kuzalishwa katika nchi mbalimbali ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

Aliwaeleza viongozi hao kuwa umuhimu wa kushirikiana katika kubadilishana mbinu, uzoefu na kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana potofu dhidi ya chanjo hizo sambamba na kuwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na janga la ugonjwa huo.

Aidha Samia alitumia mkutano huo kuziomba nchi zilizoendelea na taasisi za kifedha za kimataifa kuendelea kutoa misamaha au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni kwa nchi zinazoendelea hadi pale janga hilo litakapokwisha.

Samia alimpongeza Rais wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa SADC ambaye anachukua nafasi ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi aliyeiongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.