NA ABOUD MAHMOUD

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, katika taarab ya kusherehekea kutimia miaka 116 ya kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa.

Taarab hiyo ambayo imepangwa kufanyika Agosti 28 mwaka huu katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Akizungumza na Zanzibar Leo mwenyekiti wa sherehe Maryam Hamdan, alisema lengo la kufanya onyesho hilo ni kuonesha umahiri wa kundi hilo lililodumu kwa miaka mingi.

“Taarab ya kutimiza miaka 16 tunaitarajia kufanyika Agosti 28 mwaka huu hapo katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, na tunamtarajia Rais wetu wa Tanzania Samia kuwa mgeni rasmin,”alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kwa mwaka huu hakutokuwepo na shughuli yoyote zaidi ya hiyo taarab, ambayo itatumbuizwa na wasanii wakongwe wa kundi hilo pamoja na vijana.

“Kundi letu hili lilipotimiza miaka 100 tuliadhimisha kwa shughuli mbali mbali ikiwemo makongamano na maonyesho ya sanaa lakini kwa mwaka huu kutokana na hali tutafanya taarab peke yake,”alifafanua.

Nadi Ikhwan Safaa ikiwa na maana ya ‘ndugu wapendanao’  imeundwa rasmin mwaka 1905 ambapo mwaka huu linatimiza miaka 116 .

Kundi hilo ni miongoni kwa vikundi maarufu duniani kilichodumu kwa miaka mingi na kutoa burudani ya nyimbo za taarab asilia.