MADINA ISSA NA ASYA HASSAN

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, mama Maryam Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa tamasha la siku ya Kizimkazi ‘Kizimkazi Day’, litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Tunguu, mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid alisema sherehe hizo zitafungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassam, Agosti 28 mwaka huu.

Alisema Samia ataambatana na viongozi mbalimbali wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Zanzibar pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali kwenye hafla hiyo.

Aidha alisema kuwa katika uzinduzi huo, kutakuwepo na shughuli mbalimbali ikiwemo usafi wa mazingira, mafunzo na maonesho ya wajasiriamali 300.

Alisema kupitia tamasha hilo la kila mwaka linasaidia kuimarishwa shughuli nyingi za kimaendeleo ikiwemo elimu, miundombinu ya maji, njia za ndani, ajira kwa vijana na maendeleo ya wajasiriamali.

“Kuwepo kwa tamasha hili kunasaidia kuwapa nafasi na fursa mbalimbali wananchi wa maeneo hayo na viongozi wao kutafakari maendeleo yaliyopo pamoja na changamoto ziliyopo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na kuleta maendeleo”, alisema.

Alifahamisha kuwa mbali ya shughuli hizo tamasha hilo pia husaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya kitalii viliyopo ndani ya mkoa huo.

“Ndani ya Mkoa huo kuna fursa nyingi, hivyo kupitia tamasha hilo itakuwa chachu ya kutangazwa kwa fursa hizo pamoja na kuonekana njia zaidi za kuziendeleza ili kuzidi kuongeza kipato kitakachosaidia kuendeleza huduma za maendeleo ya kijamii,” alisema.

Hivyo, aliwaomba viongozi wa taasisi za serikali na taasisi binafsi, wawakilishi, wabunge, madiwani na viongozi wa kisiasa wa mkoa wa kusini pamoja na wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika upigaji wa chanjo hiyo.