Asema mrundikano mahabusu mzigo kwa serikali

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema jeshi la Polisi lina jukumu la kusimamia usalama, amani na utulivu ili nchi iendelee kupiga hatua katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Samia alieleza hayo jana, katika ukumbi wa jeshi la Polisi Osterbay jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao kazi kwa maofisa wakuu waandamizi wa jeshi la polisi nchini kilichobeba kaulimbiu ‘Usalama, Amani na Utulivu ni Nyezo ya Maendeleo’.

Alisema takwimu zinaonesha kuna idadi kubwa ya mahabusu jela, ambapo hadi kufikia Agosti 22, mwaka huu wamefikia 15,194 idadi ambayo inakaribia wafungwa ambao ni 16,542.

Alisema mahabusu wamekaa gerezani kwa muda tofauti wengine zaidi ya miaka mitatu na kila anayeguswa upelelezi haujakamilika, hali inayosababisha kubebesha mzigo mkubwa serikali.

Alisema amani na usalama ndio msingi wa maendeleo katika nchi, ambapo jeshi la polisi lina jukumu la kusimamia utulivu na usalama wa raia na mali zao.

Alifafanua kuwa, mwaka jana Tanzania iliingia uchumi wa kati, ambapo kuwepo kwa amani na usalama ni miongoni mwa sababu zilizoifikisha nchi hatua hiyo.

Aidha alisema ni fursa adhimu kwake kukutana na maofisa wakuu waandamizi na askari wa jeshi la polisi kutoka nchi nzima kwa pamoja, ambapo Mei 18 mwaka huu alipokwenda kuzindua kiwanda cha ushoni cha jeshi hilo huko Kurasini, Dar es Salaam, alikutana na baadhi yao.

Alieleza mafaniko mbali mbali yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika kukabiliana na uhalifu nchini, ambapo akimnukuu IGP kuwa makosa ya jinai yamepungua kutoka 56,367 mwaka 2019-2020 hadi kufikia 49,508 mwaka 2020-2021.

Alilipongeza jeshi hilo kwa hatua wanazozichukua, ambapo kipindi alipoingia madarakani baadhi ya watu walijaribu, kufanya uhalifu lakini aliwaagiza kupambana nao na hali ipo shuwari hata aliwataka waendelee kukabiliana na uhalifu.